AKAMATWA NA BASTOLA INAYODAIWA KUWA YA DK. MVUNGI

.Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia mtu mmoja (jina tunalihifadhi), kwa tuhuma za kukutwa na bastola inayodaiwa kuwa ilikuwa inamilikiwa na marehemu Dk Sengondo Mvungi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alidai jana kuwa mkazi huyo wa Kiwalani, Dar es Salaam alikutwa na bastola aina ya Revolver yenye namba BDN 6111 ikiwa na risasi 21 na baada ya kufuatilia kumbukumbu zao na kuwasiliana na familia ya Dk Mvungi walibaini kwamba ilikuwa niya mwanasheria huyo nguli.

Huyo anakuwa mtuhumiwa wa 10 kukamatwa tangu kutokea kwa tukio la kushambuliwa kulikosababisha kifo cha Mjumbe huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Dk Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Dar es Salaam usiku wa kuamkia Novemba3, mwaka huu.

Mbali ya kushambuliwa, wavamizi pia waliiba bastola, kompyuta mpakato(laptop) na simu tano za mkononi.

Kamishna Kova alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 12 jioni Mitaa ya Twiga na Jangwani alipokuwa akiangalia runinga na akifuatilia taarifa za matukio ya tukio hilo. Alisema kukamatwa kwake kulitokana na taarifa za msamaria mwema.

Alidai kwamba baada ya kukamatwa aliwaongoza polisi hadi nyumbani kwake Kiwalani ambako walikuta bastola moja na risasi hizo.


Kutoka:Mwananchi