SULTANI MAKENGA NA WAASI WENGINE WA M23 WAJISALIMISHA UGANDA

Maafisa wa Serikali ya Uganda wanasema kuwa kamanda wa kijeshi wa wapiganaji walioshindwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, DRC, M23, amejisalimisha kwa utawala wa Uganda.

Ripoti kutoka Uganda zinasema kuwa mamia ya wapiganaji wamejisalimisha pamoja na kiongozi wao, Sultani Makenga.

Wapiganaji hao wamejisalimisha katika eneo la hifadhi ya Wanyama ya Pori ya Mgahinga, kwenye mpaka wa Uganda na DRC.

Mnamo Jumanne M23 walisema kuwa wamesitisha maasi yao ya miezi 20 Mashariki mwa Congo, baada ya kutimuliwa katika ngome zao Mashariki mwa Congo na wanajeshi wa Serikali wakishirikiana na askari wa kudumisha amani wa Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo serikali za Uganda na DRC hazijaweza kuthibitsha madai haya.

Mapema wiki hii, M23 ilisema kuwa inamaliza uasi wake wa miezi kumi na tisa masaa chache baada ya majeshi ya serikali kudai ushindi dhidi ya waasi hao.

Ripoti zinasema kuwa Sultani Makenga na waasi wengine 1,700, wamesalimisha silaha zao na wanazuiliwa na jeshi la Uganda katika kambi ya jeshi ya Mgahinga, karibu na mpaka na DRC.

Mapema wiki hii, maafisa wa DRC walisemaMakenga alitoroka na kuingia Uganda au Rwanda.

Uganda imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya waasi na serikali ya DRC , ingawa hakuna mkataba wa amani umefikiwa.