TANZANIA YAENDELEA KUCHANGIA ASKARI AFRIKA

TANZANIA ni miongoni mwa nchi tano za Afrika, zilizojitolea kutoa askari wa kuunda Kikosi cha Kukabiliana na Migogoro ya Kijeshi Haraka na Mahali Popote Barani Afrika (ACIRC), kitakachoundwa kwa mujibu wa uamuzi wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana kwavyombo vya habari, ilieleza kuwa Tanzania itatoa kikosi kimoja; na nchi nyingine zilizokubali kuchangia askari ama polisi katika kikosi hicho,ni Afrika Kusini, Uganda, Algeria na Chad.

Nchi hizo zilijitokeza kushiriki katikakikosi hicho wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Majeshi wa nchi hizo, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Uamuzi wa mkutano huo uliidhinishwa na kukubaliwa na wakuu wa nchi akiwamo Rais Jakaya Kikwete. Wakuu hao walikutana Jumanne iliyopita.

"Uamuzi wa kuanzisha kikosi hicho ulitolewa na wakuu wa nchi wanachama wa AU waliokutana katika kikao chao cha 22 cha kawaida Mei, mwaka huu, mjini Addis Ababa.Kikosi hicho kitakuwa cha muda wakati Afrika inaendelea na maandalizi yake ya kuunda Jeshi la Kudumu la Afrika (ASF) na lenye uwezo wa kukabiliana na migogoro haraka na popote.

Jeshi hili litakuwa na uwezo wa kuingia nchi yoyote, chini ya AU, na hivyo wakati mwingine litatumika kutuliza migogoro katika nchi yoyote ya Afrika hata kama nchi husika haijaomba msaada wa jeshi hilo.

Jeshi hilo litakalofanya kazi yake chini ya Mfumo wa Amani na Usalama Afrika, litawezesha AU kuwa na jeshi la askari na polisi wenye uwezo na nguvu kukabiliana na mizozo ya kijeshi barani Afrika na vifaa vyake vitatolewa nchi wanachama wa Umoja huo, ambao watakuwa tayari kushiriki katika mpango huo.