Jumamosi iliyopita Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilimtangaza Samatta anayecheza soka la kulipwakatika klabu ya TP Mazembe ya DR Congo kuwa miongoni mwa wachezaji 21 watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika anayechezea timu za ndani ya bara hili.
Mshindi wa tuzo hiyo pamoja na ileya mchezaji bora wa Afrika wanatarajiwa kutangazwa Januari 9, mwakani Lagos, Nigeria.
Akizungumza jijini Dares Salaam jana, Samatta alisema anajivunia kuteuliwa kuwania tuzo hiyo lakini pia Wanatazania wanapaswa kujivunia hali hiyo kwa sababu yeye ndiye mchezaji pekee kutoka Afrika Mashariki kuingia katika kinyang'anyiro hicho ukimwondoa Victor Wanyama raia wa Kenya anayechezea Southampton ya England ambaye anawania tuzo ya Mchezaji bora wa Afrika inayohusisha wachezaji 25 wanaocheza soka nje na ndani ya Afrika.
Alisema kujituma kwake na kuzingatia maadili ndiyo siri ya mafanikio ambayo ameyapata na kuwafanya viongozi wa CAF kuona kuwa anastahili kuwania tuzo huyo.