WAFUGAJI NA WAKULIMA WAUWANA HUKO MVOMERO

MAPIGANO makali yakihusisha silaha za kisasa na jadi yamezuka kati ya wanakijiji wa Hembeti na wafugaji jamii ya Kimasai wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro na kusababisha vifo vya watu saba huku wengine 55 wakijeruhiwa vibaya.

Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, taarifa zilizolifikia gazeti hilijana jioni zilisema kuwa Kamanda wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Makao Makuu alilazimika kufika eneo hilo akiwa na kikosi cha askari kujaribu kutuliza fujo hizo licha ya awali jeshi hilo kudaiwa kutoonyesha ushirikiano.

Awali, kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Hembeti, Juma Malaja na Ofisa Mtendaji Kata, Charles Chikuni, waliokufa walikuwa wawili; Yusuph Hamad (30) mkazi wa Mkindo aliyefariki akipata matibabukatika Hospitali ya Bwagala-Turiani na mfugaji ambaye jina lake halikupatikana mara moja.

Majeruhi waliokuwa wametambuliwa ni Hamiss Hussen, Athuman Mtaalam, Kibuyo Nasoro, Mveda William, Francis Laulent na Juma Adam wakazi wa Mkindo, Muya Paulo (Hembeti), Francis William (Dihombo) na Yusuph Hamad aliyefariki akihudumiwa.

Lakini baadaye jioni, hali ilibadilika na watu watano wengine zaidi kuuawa kwa kuchinjwa huku majeruhi nao wakiongezeka kutoka 28 wa awali na kufikia 55.

Iilielezwa kuwa miili hiyo mitano ilihifadhiwa katika kituo cha afya Mvomero huku majeruhi 27 wapya nao wakapatiwa matibabu hapo. Kwamba waliouawa ni wanakijiji wanne na wafugaji wa Kimasai watatu.

Mapema, baadhi ya mashuhuda waliopiga kambi katika ofisi za tarafa na Kituo Kidogo cha Polisi Mvomero na familia zao kwa hofu ya mapigano hayo, walisema vurugu hizo zinachangiwa na rushwakukithiri kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya tarafa, wilaya na mkoa na kupuuza mawazo na mipango ya wananchi juu ya ulinzi wao na mali zao.

Zainabu Joseph na Seleman Williamambao wamelazwa hospitali ya Bwagala, walisema tukio hilo lilianza juzi saa 3:00 asubuhi katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji na Kata ya Hembeti wakati wafugaji hao wakiwa na silaha za kisasa zaidi ya saba kutaka kuwachukua kwa nguvu ng'ombe kwa kupiga risasi hovyo.

Walisema kuwa ng'ombe hao wapatao 300 walikamatwa jioni ya Oktoba 4 mwaka huu, wakiwa wameharibu chanzo cha maji Mto Dimamba, kingio la maji yanayotumika kwenye vijiji vya katahiyo na shamba la mahindi la mtu mmoja ambaye hakufahamika jina lake.

Waliongeza kuwa asubuhi ya Oktoba5, wafugaji hao walimwagiza mmojawao kuja kufanya mazungumzo ya suluhu, lakini akiwa kikaoni na viongozi wa kijiji na kata, aliwasiliana na wenzie kwa ujumbe mfupi wa simu, ambao walifika eneo hilo wakiwa na silaha hizo za kisasa.

"Tukiwa tunalinda wale ng'ombe, ghafla walikuja vijana wa Kimorani zaidi ya 15 wakiongozwa na Kafuna Kandulu na silaha za kijeshi kama saba, wakaanza kupachika magazini kwenye bunduki zao na kufyatua risasi nyingi hovyo zilizojeruhi baadhi ya watu na mimi," alisema William.

William ambaye amejeruhiwa kisogoni, shingoni, mkononi kushoto na tumboni ilikokwama risasi, alisema baada ya milio ile ya bunduki, wanakijiji walianza kutoka majumbani wakiwa na silaha za jadi zikiwemo pinde na mishale kisha kukusanyika katika eneo hilo.

Kufuatia hali hiyo, Wamasai hao walianza kuwalenga na kuwapiga risasi sehemu mbalimbali za miili yao, huku wanakijiji wakijibu kwa kuwarushia mishale iliyowasambaratisha wafugaji hao na kuanza kukimbilia porini huku wakiwarushia risasi.

Wakihusisha mgogoro huo na iliyopita, ukiwemo uliosababisha kufungwa barabara eneo la Dihombo, viongozi hao; Malaja na Chikuni kwa nyakati tofauti, walionyesha kusikitishwa na vyombo vya dola kuchelewa kuimarisha ulinzi eneo la tukio hadikufikia maafa hayo.

"Unajua wananchi walifanya kazi nzuri na kubwa sana, lakini wamekosa msaada kutoka vyombo vya dola, kwani baada ya taarifa ya kukamatwa ng'ombe wale, binafsi niliomba msaada wa nguvu ya ulinzikwa OCD na Mkuu wa Wilaya, lakini mpaka sasa hakuna hata polisi," alisema Malaja.

Kuhusu hali ya usalama katika vijiji vya kata hiyo, walisema mapigano hayo yamesababisha taharuki kubwa katika vijiji vya Hembeti, Msufini, Kwampepo, Dihombo na Mkindo ambako watu wameyakimbia makazi yao na kwenda kusikojulikana huku wengine kujihifadhi katika ofisi ya tarafa na kituo cha polisi Mvomero.

Kwa mujibu wa Dk. Mashaka Issa wahospitali ya Bwagala, hadi jana walikuwa na taarifa ya kifo cha Yusuph Hamadi (30) na juzi walipokelewa majeruhi wanane huku wengine 15 wakipokelewa jana mchana.

Alisema kuwa majeraha waliyonayoni ya kupigwa risasi na kukatwa na vitu vyenye ncha kali kama mapanga au sime.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Anthon Mtakana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustn Shilogile hawakupatikana kutoa ufafanuzi wa tukio hilo kutokana na simu zao kutokuwa hewani.


Chanzo: Tanzania daima