UN YAGOMA KUWAUNGA MKONO RUTO NA KENYATTA

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, limekatalia mbali ombi la kuahirishwa kwa kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Azimio hilo lililokuwa limependekezwa liliungwa mkono na nchi wanachama wa Muungano wa Afrika.

Viongozi hao wawili wanatuhumiwa kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa ghasia za baadaya uchaguzi mwaka 2007-08 nchini Kenya.

Kukataliwa kwa azimio hili ni changamoto ya hivi punde kwa kesi inayowakabili Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto wanaotuhumiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-08.

Lakini azimio hilo lilipata tu kura saba badala ya angalau tisa ambazo zilihitajika kupitishwa na baraza la usalama la UN.

Nchi nane wanachama wa baraza la usalama la UN, nchi wanachama wote wa ICC, Uingereza, Ufaransa na Marekani zote zilijizuia kupiga kura kuhakikisha kuwa azimio hilo halipiti.

Ilikuwa mara ya kwanza katika miaka kumi kwa baraza la usalama la UN kukosa kupigia kura azimio kama hilo bila ya kutumiwa kwa kura ya turufu na mwanachama wa kudumu wa UN.

Mataifa ya Afrika yakiongozwa na Rwanda, iliyopendekeza azimio hilo, yalikosolewa vikali kwa kupendekeza azimio hilo na kulazimisha baraza la Usalama la UN kupiga kura.

Balozi wa Guatemala katika Umoja wa Mataifa, alisema kuwa jaribio la kutaka kuahirisha kesi hiyo ilikuwa njama ya hujuma dhidi ya nchi zinazotaka kusaidia Afrika na juhudi za amani pamoja na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi katika mataifa hayo.

Kenyatta na Ruto wanatuhumiwa kwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi Kenya, mwaka 2007 ambapo takriban watu 1,100 walifariki.

Kenyatta na Ruto walichukua hatamu za uongozi baada ya uchaguzi uliofuata mwaka 2013