Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ngoro Nyengera (60) mkazi wa Kijiji cha Mirumba Tarafa ya Usevya Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi ameuwawa kwa kukatwa kolomeo na kitu chenye ncha kali nyumbani kwake wakati akiwa amelala kitandani na mume wake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo la mauwaji ya mwanamke huyo ya kusikitisha lilitokea hapo juzi majira ya saa saba na nusu usiku nyumbani kwa marehemu ambae alikuwa akiishi na mume wake aitwaye Rina Kuzenza (70) Alisema siku ya tukio marehemu alikuwa amelala na mumewe kitandani katika nyumba waliokuwa wakiishi pamoja na kijana wao aitwaye Ndura Kusenza (20) ambae yeye alikuwa akilala chumba kinachotazamana na chumba cha wazazi wake.
Kamanda Kidavashari alieleza ghafla watu wawili walivunja mlango wa chumba alichokuwa amelala marehemu na mumewe na kuingia ndani huku wakiwa na tochi kubwa mbili zenye mwanga mkali na kuwaweka chini ya ulinzi wao marehemu na mumewe.
Alisema ndipo walipomwamuru mume wa Marehemu akifunike usoni kwa shuka yake na kisha walimlazimisha alale akiwa amelala kifudifudi.
Kidavashari alieleza kuwa baada ya kulazimisha hivyo mumewe alitekeleza amri hiyo na ndipo watu hao walipoanza kumkata Ngoro Nyengera kolomeo hadi kufariki dunia Kamanda Kidavashari alisema siku za nyuma marehemu alikuwa akilalamikiwa na wanakijiji wenzake kuwa ni mshilikina na amekuwa akituhumiwa kuwaloga wanakijiji wenzake hari ambayo ilipelekea marehemu kuchukiwa na kukosa mahusiano mazuri baina yake na wanakijiji wenzake.
Alisema katika tukio hilo hakuna mtu wala watu waliokamatwa na jeshi la polisi linaendelea na upelelezi wa kuwabaini waliohusika katika mauwaji hayo ili kuweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma hii ya mauwaji ya kinyama.
Source: Katavi Yetu Blog