Waukimbia Msikiti

Kauli iliyotolewa na mbunge wa
kilindi Beatrice Shelukindo ya
kuwa msikiti wa barabara ya saba
uliopo katika manispaa ya
Dodoma unafundisha mafunzo ya
ugaidi na kareti kwa waumini
wake imeuathiri msikiti huo.

Akizungumza na Jombo Shekhe
Mohamed Awadhi wa msikiti huo
alisema kauli yake hiyo
Imewaathiri waumini wake
kutokana kuukimbia na baadhi ya
wanafunzi waliokuwa wakisoma
masomo kuhamishwa na wazazi
wao.

Awadhi alisema hivi sasa wapo
katika wakati mgumu kutokana na
waumini waliokuwa wakiswali
ndani ya msikiti huo kuamua
kuhama baada ya kutolewa kauli
ambayo wanaamini ni ya uzushi na
uchochezi kwa ajili ya kupotosha
jamii na serikali.

Shekhe huyo alisema kuwa msikiti
huo umejengwa kwa miaka mingi
na karibu baadhi ya wanaoswali ni
pamoja na viongozi wa kiserikali
wakiwemo askari toka taasisi
mbalimbali kama vile
polisi,wanajeshi,usalama na
takukuru.

“Sasa kama kweli sisi tungekuwa
tunafundisha hayo mafunzo ya
ugaidi na kareti, serikali pamoja na
waumini kutoka vyombo vya dola
kweli msikiti huo ungeachwa bila
kuchukuliwa hatua zozote ”aliuliza
Shekhe Awadhi.

Naye mlezi wa wanafunzi wa
msikiti huo wa barabara ya saba
Husseni Hamedi Fundi,alikiri
baadhi ya wazazi na walezi
kuwahamisha watoto wao
kutokana na kauli iliyotolewa na
mbunge huyo wa jimbo la Kilindi.

Fundi alisema kuwa msikiti
unapokea wanafunzi kutoka nje ya
Mkoa wa Dodoma kama vile
Kigoma,Singida,Mwanza,Pemba,
Zanzibar,Tanga na Bukoba kwa
ajili ya kujifunza lugha ya kiarabu
na elimu ya Quran.

“Lakini hivi sasa baadhi yao
wamehamishwa na wazazi, walezi
na hii yote ni kutokana na uzushi
uliotolewa na Mbunge huyo wa
Kilindi ambaye sisi kama waumini
wa msikiti huo tunaona
amepotosha jamii na serikali yetu.

''Kauli yake hiyo imetudhalilisha
sana hivyo tunaamini
Mwanamama huyo anatakiwa
kusema ukweli ukizingatia kuwa
sehemu anayoielezea ni Bunge
ambalo linalotegemewa na
Watanzania wote''.

Alisema Fundi
Kauli hiyo iliyoleta utata ilitolewa
na Mbunge wa  jimbo la Kilindi
Beatrice Shelukindo mei 4, mwaka
huu wakati akichangia bajeti ya
Wizara ya mambo ya ndani
alisema msikiti huo wa barabara
ya saba unatoa mafunzo ya ugaidi
na kareti.