Mwakyembe, Kipande wavurugana TPA

MIEZI sita baada ya Waziri wa Uchukuzi Dk. Harisson Mwakyembe, kumteua Mhandisi Madeni Kipande, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), viongozi hao kwa sasa hawaivi chungu kimoja, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Tofauti za viongozi hao imeelezwa kuwa ni baada ya Kipande kudaiwa kukaidi maagizo ya Waziri Mwakyembe.

Habari ambazo gazeti hili limezipata, zilisema kuwa  Waziri Mwakyembe amemlima barua kali ya onyo Kipande, akimtaka kusitisha uamuzi wa kuibeba kampuni ya kuhifadhi magari ya SILVER.
Kampuni hiyo imekuwa ikilalamikiwa na kampuni nyingine kwamba inapendelewa na Kipande.
Barua hiyo ya Juni 11 ambayo nakala yake tunayo, Waziri Mwakyembe amembana Kipande kuacha kuipendelea kampuni hiyo.

Katika barua hiyo yenye kichwa cha habari: ‘Kukaidi maagizo ya wizara’, Dk. Mwakyembe alimtaka Kipande atakapojibu atumie kumbukumbu namba CCB 364/505/01.
Dk. Mwakyembe ameandika katika barua hiyo kuwa amepata taarifa ya kuwapo kwa upendeleo wa moja ya makampuni ya kuhifadhi magari kinyume cha maelekezo yake aliyoyatoa Machi 3, mwaka huu alipokutana na viongozi wa wizara na wawakilishi wa ICDSVS.
“Nimefedheheshwa sana na taarifa kuwa kampuni ya kuhifadhi magari ya SILVER bado inapata ‘preferential treatment’ au bado inabebwa na TPA tofauti na kampuni nyingine za aina hiyo na kinyume kabisa cha taratibu za ushindani na kibiashara na maelekezo niliyoyatoa mbele yenu viongozi wa wizara na wawakilishi wa ICDSVS tarehe 5, Machi 2013.

“Kwa staili hii ya uongozi hatufiki, sitisheni ‘preferential treatment’ kwa Silver ‘asap’ na nipate taarifa ya utekelezaji tarehe 15 Juni, 2013 bila kukosa,” imeandikwa barua hiyo.
Nakala ya barua hiyo imepelekwa kwa Profesa Joseph Msambichaka, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Bandari.
Wakati Kipande akiandikiwa barua ya kusitisha uamuzi huo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa kaimu huyo amekuwa akilalamikiwa na makampuni tofauti hata nyingine kuamua kutoa notisi ya kukwepa kutumia Bandari ya Dar esSalaam na badala yake kuishia Mombasa.
Kikubwa kinachodaiwa na makampuni hayo kuamua kutoa notisi hiyo ni kukithiri kwa rushwa katika Bandari ya Dar es Salaam, kuwapo misuguano baina ya wafanyakazi wa bandari na wateja wakubwa wa ndani na nje ya nchi, hasa wenye meli.

Wateja wa ndani wanaodaiwa kulalamikia utendaji wa Kipande ni pamoja na Kampuni ya Tanga Cement, huku Kampuni ya Mesina kutoka nchini Italia ikielezwa kuwa tayari imeshatoa notisi ya kuacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam na badala yake kuishia Mombasa nchini Kenya kutokana na ushirikiano mdogo inaodaiwa kutoka kwa Kipande.

Januari 21  mwaka huu  Waziri Dk.  Mwakyembe aliwatimua kazi vigogo watano wa bandari ambao ni Ephraim Mgawe, naibu wake, Hamad Konshuma, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Casian Nghamilo, Kapteni Tumaini Masalo na Julius Semfuko.
Vigogo hao walidaiwa kukutwa na makosa ya uzembe uliokithiri, kushindwa kudhibiti wizi, kukosa uaminifu kupindukia, matumizi mabaya ya madaraka na kukiuka sheria.
Wakati huo Mwakyembe alisema kuwa makosa hayo yamesababisha kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji mafuta machafu bandarini na kusababisha wizi wa mafuta masafi pamoja na kutoa kibali cha utoaji mafuta hayo kinyume cha sheria.

Waziri Mwakyembe aliongeza kuwa vigogo hao kwa kushirikiana walitumia vibaya madaraka yao kwa kuingia mkataba na kampuni ya Kichina (China Communication Construction Company) bila idhini ya serikali pamoja na kupandisha mshahara kwa wafanyakazi wa bodi hiyo bila idhini ya waziri anayesimamia mamlaka hiyo.

Alisema kutokana na makosa hayo wameisababishia  Bandari ya Dar es Salaam kuwa ya  mwisho kwa utendaji kati ya bandari 36 Afrika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na DANIDA na Benki ya Dunia..
Wakati huo Dk. Mwakyembe alipofanya uamuzi huo na kumkaimisha Kipande katika nafasi ya ukurugenzi, taasisi mbalimbali za kimataifa zilionesha wasiwasi wao juu ya hali hiyo na kutahadharisha kuwa utaua uchumi wa nchi hasa katika sekta ya Bandari.

Taasisi zilizoonesha wasiwasi huo ni Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Dunia (WB) ambazo kwa nyakati tofauti zilitoa maoni yao juu ya hali hiyo.

EU kwa upande wake ambayo ilifanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam na kusifia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ilihofia mafanikio hayo kupotea.


Chanzo:Tanzania Daima