Katavi Warriors Kukipiga na Polisi Jamii

Mechi za kwanza za hatua ya tatu ya
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)
kuwania nafasi tatu za kupanda Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao
zitachezwa Jumamosi (Juni 15
mwaka huu) wakati za marudiano
zitachezwa Jumatano ya Juni 19
mwaka huu.

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imekutana leo (Juni 11 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za
michezo iliyopita na kufanya uamuzi
mbalimbali ikiwemo mechi ya
marudiano kati ya Mpwapwa Stars
na Machava FC ambayo
haikuchezwa.

Machava FC ambayo ilishinda mechi
ya kwanza iliyochezwa mjini Moshi
kwa mabao 2-0 inaendelea katika
hatua ya tatu kwa vile haikuhusika
katika kukwamisha mchezo wa
marudiano uliopangwa kuchezwa
Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dodoma (DOREFA) kiliuhamishia
mchezo huo kwenye Uwanja wa
Mgambo mjini Mpwapwa kinyume
na maelekezo ya Kamati ya
Mashindano ya TFF.

Kamati katika
kikao chake cha awali iliekeleza kuwa
mechi zote za RCL zitachezwa makao
makuu ya mikoa isipokuwa kwa
Morogoro ambapo timu ya Techfort
FC iliruhusiwa kutumia Uwanja wa
CCM Mkamba mjini Ifakara.

Hivyo timu nane zilizofuzu kucheza
raundi hiyo ni Friends Rangers ya
Dar es Salaam, Kariakoo ya Lindi,
Katavi Warriors ya Katavi, Kimondo
SC ya Mbeya, Machava ya
Kilimanjaro, Njombe Mji ya Njombe,
Polisi Jamii ya Mara na Stand United
FC ya Shinyanga.

Wakati timu nyingine zimefuzu kwa
kushinda mechi zao za raundi ya
mbili, Njombe Mji imeingia hatua
hiyo kwa kuwa timu yenye uwiano
mdogo wa kufungwa (best looser)
katika hatua ya pili.

Katika hatua hiyo mechi ni ifuatavyo;
Kariakoo vs Friends Rangers,
Machava FC vs Stand United FC,
Polisi Jamii vs Katavi Warriors, na
Kimondo SC vs Njombe Mji. Timu
zilizoanza kutajwa ndizo zinazoanzia
nyumbani.

Vilevile Kamati ya Mashindano
imeagiza Kamishna wa mechi ya
marudiano kati ya Mpwapwa Stars
vs Machava FC, Mwijage Rugakingira
wa Tanga ambaye alikwenda Uwanja
wa Mgambo badala ya Uwanja wa
Jamhuri kinyume na maelekezo ya
TFF aondolewe kwenye orodha ya
makamishna.

Pia waamuzi wa mechi hiyo ambao
nao walikwenda Mpwapwa badala
ya Dodoma Mjini wamepelekwa
Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili
ya kuchukuliwa hatua kutokana na
tukio hilo.

Kamati ya Mashindano
imekumbusha kuwa RCL ni
mashindano yanayosimamiwa na
TFF, hivyo maelekezo yoyote
kuhusiana na mashindano hayo pia
yatatoka TFF na si mahali pengine
popote. Hivyo, msimamizi wa kituoa
hana mamlaka ya kubadili uwanja.

Hatua ya nne ya RCL itachezwa kati
ya Juni 23 na 23 mwaka huu wakati
mechi za marudiano zitachezwa kati
ya Juni 29 na 30 mwaka huu.