Jela Miaka Mitatu Kwa Kumuuma Nyeti Mumewe

MAHAKAMA ya Wilaya ya Iramba
mkoani Singida umemhukumu
mwanamke mmoja mkazi wa kijiji
cha Kisana wilayani humo, Sayuni
Ramadhani (42) kwenda jela miaka
mitatu baada ya kukiri kosa la
kumng’ata mumewe sehemu
zake za siri.

Mwendesha mashitaka mkaguzi
wa polisi, Vincent Ndasa alidai
mbele ya hakimu mfawidhi wa
mahakama ya wilaya ya Iramba,
Kariho Mrisho kuwa Juni 4 mwaka
huu saa 12.00 jioni katika kijiji cha
Kisana, mshitakiwa kwa
makusudi alizing’ata kwa meno
sehemu za siri za mume wake,
Onesmo Nathania (42) na
kumsababishia maumivu.

Ndasa alidai kuwa siku ya tukio,
wanandoa hao waliporejea
nyumbani kutoka kwenye klabu
cha pombe ya kienyeji kijijini
hao, kulitokea kutokuelewana
na hivyo kuanza kugombana.

Alidai wakati wanaendelea
kupigana, Onesmo alizidiwa nguvu
na kuangushwa chini na mkewe
ambaye alifungua zipu ya suruali
na kufanikiwa kuzitoa sehemu za
siri za mumewe na kuzing'ata
nusura azitenganishe.

Mwendesha mashitaka aliendelea
kudai kuwa mlalamikaji Onesmo
alipiga yowe na majirani walifika
mara moja na kumkimbiza katika
zahanati ya kijiji kwa ajili ya
matibabu.

Mshitakiwa alipoulizwa iwapo ni
kweli alikiri kosa na akaiomba
mahakama imwonee huruma kwa
kumpa adhabu ndogo kwa kuwa
hilo lilikuwa ni kosa lake la
kwanza na kwamba anahitaji
kuwa na mumewe ili waendelee
kulea idadi kubwa ya watoto wao
kwa pamoja.

Naye mwendesha mashitaka,
Ndasa aliiomba mahakama kumpa
adhabu kali mshitakiwa ili kuwa
fundisho kwake na pia kuogofya
wanawake wanaotarajia
kuwafanyia unyama wa aina hii ya
kung’ata sehemu nyeti za waume
zao.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu
Mfawidhi Mrisho, alisema
mahakama yake imezingatia kwa
makini maombolezo ya
mshitakiwa na kufikia uamuzi wa
kutoa adhabu ya kutumikia jela
miaka mitatu.

Source:habari leo