Aliyetoa Siri za CIA Ajificha

Mwanamume aliyefichua habari za
ujasusi za Marekani, akiwa Hong
Kong, sasa ametoweka hotelini
mwake.

Edward Snowden aliambia
waandishi wa habari kuwa ameishiwa
na pesa na alisema ana hakika kuwa
maafisa wa usalama wa Marekani
watamtafuta kokote aliko.

Mfanyakazi huyo wa zamani wa CIA,
mwenye umri wa miaka 29, aliyekuwa
akifanya kazi na CIA alisema kuwa
maafisa wa kijasusi wa Marekani
walitumia mitambo maalumu
kupekua simu, barua pepe na aina
nyingine za mawasiliano kote duniani.

Alisema kuwa alifichua njma hiyo kwa
sababu aliamini ilikuwa kinyume cha
demokrasia.

Ikulu ya White House haijasema iwapo
itatoa amri ya Edward Snowden
kurudishwa nchini ili kushtakiwa kwa
kosa hilo.

Msemaji wa Ikulu, Jay
Carney, alikataa kufafanua ila akaeleza
tu kuwa uchunguzi unaendelea na
akakariri kuwa kitendo cha Snowden
kimehatarisha usalama wa Marekani.

Ingawa kuna wale ambao wamtaja
Snowden kama msaliti kwa taifa, kuna
wale waliomshangilia kama shujaa wa
kitaifa.

Maelfu ya watu wametia sahihi
katika mtandao wa Ikulu ya White
House wakitaka asamehewe kwa
makosa yo yote ambayo huenda
ameyafanya kisheria.

Huku mjadala ukiendelea iwapo
Snowden alifanya kosa au la ni
dhahiri sasa kuwa idara ya ujasusi ya
Marekani itatafuta njia nyingine ya
kukusanya habari zake za kijasusi.

Itabidi wajue iwapo kuna watu wengi
kuliko inavyodhaniwa wanaofahamu
siri za Serikali, ambao wanaweza
kuzifichua kwa umma wakati wo wote.