Shomary Kapombe Kwenda Fc Twenty Kufanya Majaribio

Beki wa kimataifa wa Tanzania
na timu ya Simba, Shomari Kapombe
anatarajiwa kuondoka nchini hivi karibuni
kwenda nchini Uholanzi kwa ajili ya majaribio ya
kucheza soka la kulipwa katika klabu ya FC
Twente.

Kapombe mwanasoka bora wa mwaka huu
amekuwa na mafanikio makubwa tangu
alipojiunga na Simba akitokea Polisi Morogoro
miaka mitatu iliyopita kwa kuisaidia Simba
kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Hivi sasa Kapombe anatarajiwa kwenda kufanya
majaribio katika klabu ya FC Twente, ambayo
ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uholanzi katika
msimu wa 2009-10, pia ilifanikiwa kucheza hatua
ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika
msimu huo.

Katika msimu uliopita FC Twente imemaliza
katika nafasi ya sita katika Ligi Kuu ya Uholanzi
ikiwa na pointi 62, huku Ajax wakiwa mabingwa
kwa pointi 76.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Swed
Nkwabi akizungumza na Mwananchi jana jijini
Dar es Salaam alisema,"timu atakayokwenda
kufanya majaribio Kapombe huko nchini
Uholanzi ni FC Twente, suala la ataondoka lini
kwenda kufanya majaribio tutawaambia safari
itakapokuwa tayari."

Akizungumza katika kipindi cha Spoti Leo cha
Radio One juzi, Mwenyekiti wa Simba, Ismail
Aden Rage alisema amekwishatoa kibali kwa
Kapombe kuondoka nchini siku yoyote kuanzia
sasa kwa ajili ya kufanya majaribio nchini
Uholanzi.

Alisema Kapombe alitakiwa kuondoka mapema kwa ajili ya majaribio hayo, lakini mpaka hivi sasa
amechelewa zaidi ya siku saba kutokana na kuisubiri mechi ya Taifa Stsr dhidi ya Ivory Coast ya kuwania
kufuzu Fainali za Kombe la Dunia imalizike.

Katika mchezo huo wa kusaka kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014, dhidi ya Ivory Coast,
Kapombe alichangia kupatikana kwa bao la pili la Taifa Stars lililofungwa na Thomas Ulimwengu.

Akizungumzia safari hiyo ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka nchini Uholanzi, Kapombe
alisema mimi nimeambiwa kuhusu safari hiyo, lakini sijui ni timu gani ninayokwenda kufanya nayo
majaribio."

"Sijui ni lini nitaondoka kwa sababu hivi sasa mimi ni majeruhi, niliumia katika mchezo dhidi ya Ivory
Coast na nimetakiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja au mbili,"alisema Kapombe.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alitoa ushauri kwa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) kumruhusu mchezaji huyo kwenda kwenye majaribio hayo kwani akifanikiwa itakuwa ni faida.

''Unajua kwa sasa Taifa Stars wanajiandaa na
michuano ya fainali za wachezaji wanaocheza
ligi za ndani ya Afrika (CHAN), TFF wanaweza
kumzuia mchezaji huyo kwa ajili ya maandalizi
hayo, nawaomba wasifanye hivyo,"alisema
Rage.

Hii ni mara ya pili kwa Rage kutangaza kuwa
Kapombe anatakiwa kufanya majaribio nje
baada ya kumuhusisha beki huyo na winga
Ramadhani Singano kutakiwa kufanya majaribio
katika klabu ya Sunderland ya England.

Mapema mwezi Februari, Rage alikaririwa
akisema Kapombe na Singano wataondoka
kwenda London mwishoni mwa msimu wa ligi.


Chanzo: Mwananchi.co.tz