Dar es Salaam. Licha ya ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama kutarajiwa kufikia katika hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo atakapowasili nchini Julai Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa tahadhari ya vyakula ambavyo hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni pamoja na kutumia maji ya bomba.
Mbali na tahadhari hiyo, ziara hiyo ya Obama
itakuwa na ulinzi mkubwa ambao pengine haujawahi kutokea katika historia
ya viongozi wa nje wanaotembelea Tanzania kwani utahusisha idadi kubwa
ya magari, ndege za kijeshi na meli kubwa ya kivita ambazo zitakuwa
zikifanya doria karibu na pwani ya Tanzania.
Tahadhari za matumizi ya chakula, maji na
nyinginezo zimetolewa katika nchi zote tatu za Afrika ambazo Obama
atatembelea, kila moja kwa jinsi Wamarekani hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Ulinzi
Vyombo vya usalama vya Marekani vimejipanga
kuhakikisha ziara ya kiongozi huyo haivurugwi kwa namna yoyote ile.
Tayari ndege za jeshi zilizobeba magari ya akiba 56, yakiwemo 14 aina ya
‘Cadillac One’ maalumu kwa ajili ya kiongozi huyo, yamewasili katika
nchi hizo tatu za Afrika atakazotembelea.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post la
Marekani, ndege hizo pia zimebeba malori matatu ambayo yamesheheni
karatasi maalumu za kuzuia risasi kupenya kwenye vioo, zitakazobandikwa
kwenye madirisha ya hoteli ambazo Rais Obama na ujumbe wake watafikia.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mamia ya mashushushu wa
Marekani tayari wako katika nchi hizo. Meli maalumu za kubeba ndege za
kivita, maarufu kwa jina la ‘amphibious ship,’ ikiwa na hospitali
maalumu na yenye vifaa vyote itaweka nanga baharini, jirani na nchi
atakayokuwa Rais Obama, tayari kukabiliana na dharura yoyote
itakayotokea. Gazeti hilo liliandika kuwa ndege za kivita za Marekani
zitakuwa zikipeana zamu kufanya doria kwa saa 24, katika anga la nchi
ambayo Rais Obama atakuwepo, iwapo ndege za ‘adui’ zitakaribia eneo
linaloitwa ‘anga ya rais.’ Kwa mujibu wa gazeti hilo, ziara ya Rais
Obama aliyoifanya hivi karibuni katika nchi za Ujerumani na Ireland
Kaskazini, japo kulikuwa na gharama kwa walinzi, lakini safari za nchi
za Afrika zimeelezwa kuwa na gharama kubwa zaidi.
Tahadhari
Kwa mujibu wa taarifa ya maelekezo ya Ikulu ya
Marekani, ambayo Mwananchi imepata nakala yake, watu watakaokuwa kwenye
msafara wa Obama wametakiwa kutotumia kachumbari. Pia imewataka kutumia
maji ya chupa zaidi.
“Kutokana na mfumo wa maji uliopo, tunashauri watu
wetu kutumia maji ya chupa zaidi kwa kunywa na hata kwa kupiga mswaki,”
ilisema taarifa hiyo.
Kwa kuelewa fika tatizo la ugonjwa wa malaria
nchini, ujumbe wa Obama umeshauriwa kutumia dawa ya mbu ya kupaka na
kupuliza inayoitwa Deet.
Deet ni dawa maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti
ikiwamo ya kupaka na kupuliza na imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani
kwenye vita mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na
raia mwaka 1957.
ATM nazo noma
Pia watu watakaokuwa kwenye msafara wa Rais Obama
wametakiwa kuhakikisha wanatumia mashine za kutolea fedha (ATM) zilizoko
karibu na hoteli watakazofikia.
“Kuna tatizo la uhalifu kwa hiyo siyo vizuri
kutumia ATM ambazo ziko katika sehemu zisizo salama. Pia katika kipindi
watakachokuwa Tanzania watu wanapaswa kutumia teksi ambazo
zimeidhinishwa na hoteli.
“Pia siyo vizuri kuacha kompyuta ya fedha kwenye
vyumba mtakavyolala. Pia kina mama wanapaswa kuchukua tahadhari ya
mabegi yao watakapokuwa wanapita mitaani,” ilitahadharisha taarifa hiyo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi