Rasimu ya Katiba Mpya: Mgombea Binafsi Apendekezwa

Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini
Tanzania, imependekeza wawepo
wagombea huru katika ngazi za
uchaguzi mbalimbali nchini humo.

Hayo ni miongoni mwa mapendekezo
yaliyotangazwa jijini Dar es salaam na
Mwenyeketi wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakati
wa uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya
Katiba Mpya.

Jaji Warioba amesema pia wapo
wananchi waliopendekeza kwamba,
wagombea huru waruhusiwe
kugombea nafasi zote isipokuwa
nafasi ya urais.

Jaji Warioba amesema
tume ilipitia maoni hayo na
kupendekeza kwamba, wagombea
huru waruhusiwe kugombea nafasi
zote kuanzia ngazi ya Mwenyekiti wa
Mtaa hadi nafasi ya Urais.

Kadhalika Jaji Warioba amesema,
Tume pia imependekeza kwamba,
mgombea yeyote wa urais ili athibitike
kuwa ni mshindi atalazimika kupata
zaidi ya asilimia hamsini ya kura, na
kwamba endapo mgombea
hatafanikiwa kupata asilimia hamsini
uchaguzi utarudiwa kwa kuangalia
wagombea wawili waliopata kura
nyingi.

Mapendekezo mengine
yaliyotangazwa na Tume ni pamoja na
kuwepo kwa serikali tatu yaani ya
Bara,Zanzibar na ile ya Shirikisho.

Pia tume imependekeza kuwa, Bunge
la Muungano liwe na jumla ya
Wabunge 75, hamsini kutoka Bara,
ishirini kutoka visiwani na watano
wateuliwe na Rais kutoka makundi
maalum ya walemavu.

Mapendekezo mengine ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ni pamoja na
Rais kubakia na madaraka yake ya
uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu,
lakini uteuzi wa ngazi za chini uachiwe
Tume ya Utumishi.

Imeeleza kwamba, Rais mara baada
ya kufanya uteuzi wa viongozi wa
ngazi za juu wakiwemo, mawaziri,
manaibu waziri, jaji mkuu na naibu jaji
mkuu, viongozi hao watalazimika
kuthibitishwa na Bunge.