Ngono Ya Mdomo Inasababisha Saratani

Saratani imeendelea
kuwa tishio hapa nchini huku hofu
ikiendelea kuikumba jamii kutokana na
wataalamu wa afya kushindwa
kufahamu tiba halisi ya maradhi hayo
hatari.

Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road zinaonyesha ongezeko la
saratani ya mdomo na koo kwa kiasi
kikubwa kutoka kesi 167 mwaka 2006
hadi 277 mwaka 2012.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Ocean
road, Julius Mwaiselage anaeleza kuwa
watanzania wasipende kuiga mambo
ambayo si sahihi bila kujua madhara
yake kama kufanya mapenzi kwa njia
ya mdomo. "Saratani ya mdomo ipo,
na nyingine zinasababishwa na zinaa "
anasema Dk Mwaiselage
Tafiti mbalimbali zimewahi kufanyika
nchini na kubaini kuwepo kwa
ongezeko la saratani ya mdomo.

Utafiti
uliofanywa na Dk Innocent Mosha wa
Kitengo cha Patholojia cha Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH), umebaini
aina za saratani 1,594, kati ya hizo 509
zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003
pekee.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kati
ya saratani 509 za mdomo, saratani
242 zilisababishwa na Virusi vya
Human Papiloma ambavyo hutokana
na zinaa.

"Ninachojua mimi ni kuwa Virusi vya
HPV husababishwa na magonjwa ya
zinaa, hivyo mtu anayeugua saratani ya
aina hiyo, imetokana na zinaa,"
anasema Dk Mosha.

Takwimu hizo ni zile zilizopatikana kwa
watu waliokwenda kufanyiwa
uchunguzi katika Mkoa wa Dar es
Salaam pekee.

Dk Mosha anasema kuwa wanaume
ndiyo huathiriwa zaidi na saratani ya
mdomo ambapo kwa hapa nchini,
asilimia 53 ya wanaume waliofika MNH
kwa ajili ya vipimo, walibainika kuugua
saratani hiyo, huku wanawake wakiwa
ni asilimia 47.

Utafiti kama huo ulifanywa pia na Dk
Amos Mwakigonja, mkuu wa Idara ya
Patholojia katika Chuo Kikuu cha Tiba
cha Muhimbili (MUHAS).

Dk Mwakigonja alifanya utafiti wa
saratani ya mdomo aina ya Kaposi's
Sarcoma ambapo wagonjwa 78
walibainika na saratani hiyo kuanzia
mwaka 1990 hadi 2003.
"Saratani za
mdomo zipo za aina nyingi na
zimetofautiana kulingana na
visababishi vyake," anasema Dk
Mwakigonja.

Katika utafiti wake Dk Mwakigonja
alibaini kuwa wanawake wengi
walikuwa na saratani ya mdomo aina
ya Kaposi's Sarcoma kuliko wanaume.

Hata hivyo, utafiti huo ulionyesha kuwa
asilimia 50 ya wanaume walikuwa na
saratani ya mdomo hatari zaidi
(systemic) kuliko wanawake ambao ni
asilimia 37.

Mapenzi kwa mdomo husababisha
maradhi
Dk Mwakigonja anasema kuwa
mapenzi yoyote kwa njia ya mdomo
lazima yasababishe maradhi ya zinaa
iwapo mmoja ameambukizwa.

Pia anasema kwamba sampuli nyingi
za wanaume wanaojihusisha na
mapenzi na wanaume wenzao
(mashoga) zilibainika na saratani ya
mdomo.

Utafiti huo ni sehemu ya utafiti wa
Shahada ya Uzamivu ambao
ulionyesha kuwa wagonjwa wengi wa
saratani ya mdomo walikuwa ni
wanaume wenye umri wa miaka kati ya
38 na kuendelea na wanawake ni 31.

Ufatiti wa WHO Tanzania

Shirika la Afya Duniani (WHO) pia
lilifanya utafiti mwaka 2010 nchini kwa
kushirikiana na Kituo cha Taarifa za
HPV, ambapo ilibainika kuwa asilimia
20 ya saratani za koo na mdomo nchini
zinasababishwa na ufanyaji wa
mapenzi kwa njia ya mdomo.

Taarifa hizo za WHO zinaeleza kuwa
wanaume 747 hugundulika na saratani
ya mdomo kila mwaka wakati
wanawake 472 hubainika na saratani
hiyo pia.

Wakati huohuo, wanaume
wanaopoteza maisha kutokana na
saratani hiyo ni 444, kwa mwaka na
wanawake ni 270, kwa mwaka.

Utafiti wa WHO umebaini kuwa saratani
ya mdomo inashika nafasi ya sita katika
aina 24 za saratani 24 zinazoisumbua
zaidi Tanzania.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanaume
wanaoathirika zaidi ni wenye umri wa
kati ya miaka 15 na 55, ambao tayari
wameshaanza kujihusisha na ngono.

Kama maradhi mengine ya
kuambukiza, Virusi vya HPV
huambukizwa kwa urahisi zaidi kutoka
kwa wanawake kwenda kwa wanaume
kuliko kutoka kwa wanaume kwenda
kwa wanawake.

Utafiti huo uliodhaminiwa na mfuko wa
Bill na Melinda Gates na Kituo cha
Saratani na Mpango wa Utafiti wa
Taasisi ya ICO unaeleza kuwa mitandao
ya kijamii na picha za ngono ndiyo
chanzo cha watu wengi kuiga ufanyaji
wa mapenzi ya aina hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York
Times, tafiti zimefanyika na kubaini
kuwa asilimia 70 ya wagonjwa
wanaobainika na saratani ya koo na
mdomo duniani, husababishwa na
Virusi vya Human Pappiloma
vinavyotokana na magonjwa ya zinaa.

Tafiti hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa
wengi wanaogundulika na saratani
hiyo ni wanaume wenye umri wa kati,
wenye uwezo wa kifedha, wasiovuta
sigara wala siyo walevi waliokubuhu.

Utafiti huo ulibaini kuwa wanaume
wapo hatarini zaidi kupata saratani ya
koo inayosababishwa na Virusi vya
HPV.

Miaka ya 80, idadi ndogo ya watu
waliougua saratani ya koo
walihusishwa na maambukizi ya Virusi
vya HPV.

Kihistoria, watu waliobainika na
ugonjwa huo, ni wenye umri wa miaka
70 kwenda juu ambao walikuwa ni
wale walevi waliokubuhu na wavuta
sigara.

Ilielezwa kuwa Virusi vya HPV vipo kwa
wingi kiasi ambacho watu wazima
wanaojihusisha na ngono ya aina
yeyote ile, huweza kupata maambukizi
ya zinaa hata kama siyo saratani.

Hata hivyo ilibainishwa kuwa saratani
isababishwayo na virusi vya HPV ni
rahisi kuitibu kuliko saratani ya koo
isababishwayo na tumbaku au pombe
kali.

Virusi vya HPV ni nini?
Kwa jina la jumla, saratani ya koo au
mdomo huitwa saratani ya kichwa na
shingo. (Neck and Head Cancer)
HPV ni miongoni mwa virusi hatari zaidi
duniani visababishwavyo na magonjwa
ya zinaa na vinaweza kuathiri sehemu
mbalimbali za mwili.

Zipo aina zaidi ya 120 za HPV, baadhi
huweza kuzalisha usugu (warts)
ambazo si saratani katika sehemu za
siri, mikononi na miguuni.

Maambukizi ya HPV hufanyika kwa
urahisi, hata kwa kugusana ngozi au
majimaji, huku maambukizi mengine
yakisababishwa na ngono.

Virusi hatari na vinavyosababisha
saratani ni HPV-16, HPV-18, HPV-31 na
HPV 45.

Aina hii ya Virusi vya HPV husababisha
saratani ambapo uvimbe waweza
kujitokeza kwa ndani na unaweza
usionekane ukilinganisha na vivimbe
vingine vya saratani.

Wataalamu wanasema HPV-16 na
HPV-18 inahusishwa zaidi na saratani
ya shingo ya kizazi na endapo mapenzi
kwa njia ya mdomo yatafanywa na mtu
mwenye uambukizo huu ni rahisi
kuambukizwa.