Kesi ya Ruto Kuhamishiwa Tanzania au Kenya

Kesi inayomkabili
makamu wa Rais wa Kenya, William
Ruto kwenye Mahakama ya
Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huenda
ikahamishiwa nchini Tanzani au
Kenya.

Hiyo inatokana na uamuzi
unaotajwa kufikiwa na majaji wa ICC
ambao wametoa mapendekezo
wakimtaka Rais wa ICC aangalie
umuhimu na kutoa ruhusa ya kesi
hiyo kusikiliziwa nchini Kenya au
kama ikishindikana basi isikiliziwe
nchini Tanzania.

Uamuzi huo unaweza pia
kusababisha athari za kuichochea
mahakama hiyo kuhamisha pia kesi
ya aina hiyo inayomhusu Rais
Uhuru Kenyatta ambaye pia
mawakili wake wameomba kesi
dhidi yake ihamishiwe nchini Kenya
au Tanzania.

Ruto pamoja na mtuhumiwa
mwenzake, aliyekuwa mtangazaji wa
Redio, Joshua Arap Sang
wanakabiliwa na mashtaka kadhaa
ya uhalifu dhidi ya ubinadamu
wakidaiwa kuhusika kuchochea
vurugu za baada ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2007 zilizosababisha vifo
vya zaidi ya watu 1,000.

Mapendekezo hayo yametokana na
ombi hilo lililotumwa Januari 24
mwaka huu ambalo lilikuwa bado
likiendelea kujadiliwa n amamlaka
zinazohusika kwenye mahakama
hiyo.

Februari mwaka huu, Mwendesha
mashtaka mkuu wa ICC, Fatou
Bensouda aliieleza mahakama hiyo
kwamba hana pingamizi iwapo
itakubalika kesi hiyo isikiliziwe
Tanzania au Kenya.

Hata hivyo mahakama hiyo ilieleza
kuwa mapendekezo hayo bado
yanaendelea kujadiliwa kwa mujibu
wa taratibu zilizowekwa na
mahakama hiyo.

Hata hivyo, jana ICC ilitoa taarifa
ikisema kesi dhidi ya Ruto
anayetuhumiwa kufanya makosa ya
uhalifu dhidi ya binadamu itaanza
Septemba 10 mwaka huu.

Taarifa hiyo imesema majaji
wameamua kupanga tarehe ya
kusikilizwa kesi hiyo mapema zaidi
kuliko ilivyopangwa awali.

Rais Kenyatta na naibu wake
wanahitajika kupandishwa kizimbani
ili kujibu mashtaka yanayowakabili
ya uhalifu dhidi ya ubinadamu,
makosa ambayo waliyafanya wakati
wa vurugu zilizotokea baada ya
uchaguzi mkuu wa Rais wa mwaka
2007/08.