Rasimu ya Katiba Mpya

1. UTANGULIZI

Ndugu Wananchi,
Awali ya yote namshukuru
mwenyezi mungu kwa
kutuwezesha kufikia hatua hii ya
leo ya kuzindua Rasimu ya
Katiba. pia, niwashukuru ninyi
nyote mliohudhuria halfa hii
ikiwa ni mwendelezo wa
mchakato muhimu wa
Mabadiliko ya Katiba ya nchi
yetu.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ilipitishwa Bungeni Novemba,
2011 na kufanyiwa mabadiliko
Februari, 2012. Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliundwa
kwa mujibu wa Kifungu 6(1) cha
sheria hiyo (Cap.83). Wajumbe 34
wa Tume waliteuliwa na
kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete, mwezi Aprili,
2012. Kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Tume
imepewa miezi kumi na minane
kukamilisha kazi yake kuanzia
siku ilipoanza kazi rasmi ambayo
ilikuwa Mei 2, 2012.

Tume iliandaa ratiba ya
utekelezaji wa majukumu yake.

Kufuatana na ratiba hiyo Tume
ilijipanga kukusanya maoni ya
wananchi katika kipindi cha miezi
mitano kuanzia Mwezi Julai hadi
Disemba, 2012. Kazi hiyo
ilifanywa kama tulivyopanga.

Tume ilijigawa katika makundi na
ilitembelea mkoa yote
thelathini.
Tume ilifanya mikutano 1,942
ambayo ilihudhuriwa na
wananchi wapatao 1,365,337
ambao kati ya hao wananchi
333,537 walitoa maoni ama kwa
mazungumzo ya ana kwa ana au
kwa maandishi. Tume pia ilipata
maoni ya wananchi wengi, wa
ndani na nje ya nchi kwa njia
mbali mbali kama vile; Mikutano
ya hadhara, Fomu maalum za
Tume, barua kupitia Masanduku
ya Barua ya Tume, Mitandao ya
Kijamii ya barua pepe; facebook
ya Tume, Tovuti ya Tume; Makala
mbalimbali kutoka kwenye
magazeti na ujumbe mfupi wa
simu.

Tume ilitumia mwezi Januari,
2013 kukusanya maoni ya
makundi mbali mbali katika
jamii, ikiwa ni pamoja na vyama
vya siasa, taasisi za Serikali,
taasisi za dini, wakulima,
wafugaji, wafanyakazi, asasi za
kiraia na kadhalika. Makundi
zaidi ya 160 yalikutana na Tume
na kutoa maoni. Tume pia ilipata
maoni ya viongozi wa juu wa
Serikali walioko madarakani na
waliostaafu. Kwa jumla viongozi
43walitoa maoni.

Tume ilipanga kutumia miezi
mitatu ya Februari, Machi na
Aprili kuchambua maoni ya
wananchi na kuandaa Rasimu ya
Katiba. Lakini tuligundua
kwamba maoni tuliyopata
yalikuwa mengi sana, na pamoja
na matumizi ya teknolojia ya
kisasa, tulitambua umuhimu wa
kuongeza muda hadi mwisho wa
mwezi Mei, Maoni ya wananchi
yaligusa mambo yote yanayohusu
Katiba na mengi ya maoni hayo
yalikinzana. Aidha, baadhi ya
maoni yaligusia masuala ya
Kisera, Kisheria na Kiutendaji.

Tulifanya uchambuzi makini na
wa ndani wa maoni hayo na kazi
hiyo tumeikamilisha na rasimu
imeandaliwa na Tume na leo
tupo hapa kwa ajili ya kuizindua,
ambapo Wananchi watapata
nafasi ya kuisoma. Kwa leo, kwa
niaba ya Tume, napenda kutaja
maeneo machache tu ambayo
tunayapendekeza.

IBARA ZINAZOPENDEKEZWA
KWENYE RASIMU YA KATIBA

Ndugu Wananchi,
Katiba yetu ya sasa ina ibara 152.

Tume ilifanya jitihada kubwa
sana kuandaa rasimu ambayo
siyo ndefu. Lakini katika hali
halisi haikuwezekana. Rasimu ya
Katiba tunayopendekeza ina
ibara 240.

MISINGI MIKUU YA TAIFA

Utangulizi wa Katiba ya sasa ndio
unaobeba misingi mikuu ya Taifa
ambayo ni Uhuru, Haki, Udugu na
Amani. Tume inaamini kwamba
misingi hii ni mizito na inastahili
kubaki kwenye Katiba mpya.
Hata hivyo, Tume imeona ni
busara kuongeza misingi mingine
mitatu ya Usawa, Umoja na
Mshikamano. Hivyo, Tume
imependekeza Katiba iwe na
Misingi Mikuu saba ya
Taifa;yaani; Uhuru, Haki, Udugu,
Usawa, Umoja, Amani na
Mshikamano.

TUNU ZA TAIFA

Katiba yetu ya sasa haina sehemu
inayoelezea tunu za Taifa
(National Values). Wananchi
wengi walitoa maoni kwamba
Katiba itaje Tunu za Taifa.

Tume
imependekeza Tunu zifuatazo
zitajwe ndani ya Katiba.

Tunu
hizo ni;- Utu, Uzalendo, Uadilifu,
Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na
Lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.

MALENGO YA TAIFA

Tume ilipozunguka nchi nzima
wananchi walizungumzia sana
kuhusu malengo ya taifa.
Walitaka Katiba ionyeshe dira ya
taifa. Wananchi wanayo ndoto
yao ya Tanzania ya kesho na
kesho kutwa. Kwa kuzingatia
maoni ya wananchi, kuna sura
nzima inayohusu Malengo
mahsusi na ya msingi ya
mwelekeo wa shughuli za
Kiserikali na Sera za Kitaifa.

Rasimu ya Katiba inaeleza kuwa
Malengo ya Kitaifa yaliyoainishwa
ndani ya Rasimu yatakuwa ni
Mwongozo kwa Serikali, Bunge,
Mahakama, Vyama vya Siasa,
Taasisi na Mamlaka nyingine, na
kwa kila mwananchi katika
matumizi au kutafsiri Masharti ya
Katiba au Sheria nyingine za
Nchi.

Kwa msingi huo, Tume
imependekeza malengo makuu
ya taifa yapanuliwe kwa
mpangilio wa kuonesha malengo
ya kisiasa, kiuchumi, kijamii,
kiutamaduni, kimazingira na sera
ya mambo ya nje. Malengo hayo
yameingizwa kwenye Rasimu ya
Katiba.

VYOMBO VYA KIKATIBA

Wananchi walizungumzia suala la
kubainishwa kwa vyombo vya
Kikatiba na kuingizwa kwenye
Katiba ili viwe na nguvu ya
Kikatiba katika utekelezaji wa
majukumu yao. Tume
imependekeza baadhi ya vyombo
vifuatavyo viwe vya Kikatiba;

Tume ya Uhusiano na Uratibu wa
Serikali, Baraza la Mawaziri,
Kamati Maalum ya Makatibu
Wakuu na Sekretarieti ya Baraza
la Mawaziri; Baraza la Ulinzi na
Usalama la Taifa, Tume Huru ya
Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa
Mahakama, Tume ya Utumishi wa
Umma, Tume ya Maadili ya
Uongozi na Uwajibikaji, Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala
Bora

MAADILI YA VIONGOZI NA
MIIKO YA UONGOZI

Wananchi wengi pia
walizungumzia kwa upana sana
kuhusu maadili na miiko ya
Viongozi, kwa kuzingatia maoni
ya wananchi Tume inapendekeza
maadili ya viongozi wa umma,
pamoja na miiko ya uongozi
yawekwe kwenye Katiba. Tume
pia imependekeza kuwa
Sekretariati ya Maadili
ibadilishwe kuwa Tume yenye
mamlaka makubwa ya kusimamia
maadili ya viongozi wanaovunja
miiko ya uongozi.

HAKI ZA BINADAMU

Kuhusu haki za binadamu
wananchi walitaka haki hizi
ziimarishwe na kusiwe na
vikwazo visivyo vya lazima.

Tume
imependekeza mabadiliko katika
baadhi ya haki za binadamu kwa
madhumuni ya kuziimarisha.

Moja ya mabadiliko hayo ni
kuhusu uhuru wa mwananchi
kushiriki shughuli za umma.

Tume inapendekeza kwamba
vikwazo vilivyowekwa kuzuia
mgombea huru viondolewe. Kwa
maana nyingine Tume
inapendekeza mgombea binafsi
aruhusiwe.

Tume pia, inapendekeza haki
mpya ziingizwe kwenye Katiba
ikiwa ni pamoja na haki ya
wafanyakazi, , haki ya mtoto,
haki za Watu wenye Ulemavu,
Haki za Wanawake, Haki za
Wazee, Haki za Makundi Madogo
katika Jamii, Haki ya Elimu na
Kujifunza, Haki ya kupata habari,
Haki na uhuru wa habari na
vyombo vya habari na kadhalika.

URAIA

Wananchi wengi walipendekeza
kuwa suala la Uraia libainishwe
wazi kwenye Katiba. Tume
imependekeza kwa kutaja Raia
wa Jamhuri ya Muungano na haki
zake.

MIKOPO NA DENI LA TAIFA

Ndugu Wananchi,
Wananchi walizungumzia suala la
uwepo wa Ukomo wa nchi
kukopa na uwepo wa utaratibu
wa kulipa Deni la Taifa ili
kuilinda Nchi isiwe na deni
kubwa. Kwa kuzingatia maoni ya
Wananchi, Tume imependekeza
kuwa, Serikali itawajibika kutoa
taarifa Bungeni kuhusu Mikopo
kwa kuainisha kiasi cha deni
lililopo, riba yake na matumizi ya
fedha za Mikopo na utaratibu wa
kulipa Madeni ya Taifa.

MFUMO WA UTAWALA

Kuhusu utawala, Tume
inapendekeza Tanzania iendelee
na mfumo wa Jamhuri kwa maana
ya nchi inayoongozwa na Rais
Mtendaji ambaye ni Mkuu wa
nchi, Kiongozi wa Serikali na
Amiri Jeshi Mkuu.

UCHAGUZI WA RAIS

Umri wa kugombea Urais
Tume ilipokea maoni
yanayokinzana kuhusu umri wa
mwananchi kugombea Urais.

Baadhi walipendekeza mtu
akishakuwa na sifa ya kupiga
kura awe pia na sifa ya
kugombea Urais. Umri wa mtu
kuruhusiwa kupiga kura ni miaka
18.

Wengine walipendekeza umri
uliopo kwenye Katiba wa mtu
kugombea Urais, yaani kuanzia
miaka 40 na kuendelea,
uendelee kubaki kama ulivyo.

Wengine walisema Umri wa mtu
kuruhusiwa kugombea Urais uwe
miaka 35 au miaka 50 na
kuendelea.

Tume imeyachambua maoni yote
hayo, ikafanya utafiti kwa kupitia
Katiba za Nchi zingine na uhalisia
wa watu wanaogombea na
kuchaguliwa kuwa Marais katika
Nchi mbalimbali Duniani ambazo
zingine zimeruhusu wagombea
wa nafasi ya Urais kuwa na umri
chini ya miaka 40.

Wengi walioomba kugombea
nafasi hiyo walikuwa na umri wa
miaka 40 au zaidi.

Kwa kuzingatia maoni ya
wananchi, utafiti na hali halisi,
Tume inapendekeza Rais
aendelea kuchaguliwa na
wananchi na pamoja na sifa
nyingine, mtu anayeomba urais
asiwe chini ya miaka 40.

Uchaguzi wa Rais itakuwa kama
ilivyo sasa, yaani mgombea Urais
atakuwa na mgombea mwenza
kwa utaratibu kama ilivyo sasa.

Isipokuwa, Tume imependekeza
Mgombea Urais anaweza
kupendekezwa na Chama cha
Siasa au kuwa Mgombea Huru.

Mgombea wa nafasi ya Rais
atatangazwa kuwa mshindi iwapo
atakuwa amepata kura zaidi ya
asilimia hamsini ya kura zote
zilizopigwa.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi
wa Rais yanaweza kulalamikiwa
Mahakamani, lakini siyo kila mtu
anaweza kufungua kesi.

Wanaoweza kufungua kesi ni
wagombea Urais. Aidha, ni
Mahakama ya Juu pekee ndiyo
itakuwa na Mamlaka na uwezo
wa kusikiliza malalamiko kuhusu
matokeo ya uchaguzi wa Rais na
shauri lazima liamuliwe ndani ya
mwezi mmoja, yaani siku
therathini.
Rais aliyeshinda ataapishwa siku
thelathini tangu alipotangazwa
kuwa mshindi au kuthibitishwa
na Mahakama.

MADARAKA YA RAIS

Ndugu Wananchi,
Tume inapendekeza kwamba,
Rais abaki na madaraka ya uteuzi
wa viongozi wa ngazi za juu. Hata
hivyo inapendekezwa Rais
ashirikiane na taasisi na vyombo
vingine katika uteuzi. Kwa
mfano:
Uteuzi wa Mawaziri na Manaibu
Waziri, Rais atateua na Bunge
litathibitisha.

Kuhusu Jaji Mkuu na Naibu Jaji
Mkuu Rais atawateua kutokana
na majina ya watu
waliopendekezwa na Tume ya
Uutumishi wa Mahakama na
baada ya hapo Bunge
litathibitisha.

Kuhusu Wakuu wa vyombo vya
Ulinzi na Usalama
inapendekezwa kianzishwe
chombo kipya kitakachoitwa
Baraza la Ulinzi na Usalama la
Taifa, ambalo kati ya majukumu
yake itakuwa ni kumshauri Rais
kuhusu uteuzi wa Wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama.

Kuhusu Makatibu Wakuu na
Naibu Makatibu Wakuu
watateuliwa na Rais kutokana na
mapendekezo ya Tume ya
Utumishi wa Umma.

KINGA YA RAIS

Tume baada ya kupitia maoni ya
Wananchi, inapendekeza Rais
abaki na kinga kama ilivyo sasa
na anaweza kushitakiwa na
Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.

IDADI YA MAWAZIRI

Inapendekezwa Rais aunde
Serikali ndogo iliyo na Mawaziri
wasiozidi kumi na tano na
mawaziri hao wasiwe wabunge.

Mawaziri hawatahudhuria vikao
vya Bunge isipokuwa kama
watahitajika kutoa ufafanuzi
kwenye kamati za Bunge.

BUNGE

Ndugu Wananchi,
Kuhusu Bunge kutakuwa na
wabunge wa aina mbili

Kutakuwa na Wabunge wa
kuchaguliwa na wabunge watano
wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha
Watu wenye Ulemavu.

Kila Jimbo la Uchaguzi litakuwa na
Wabunge Wawili mmoja
mwanamke na mwingine
mwanamume.

Tume inapendekeza kwamba,
Mbunge akifukuzwa na Chama
cha Siasa abaki kuwa Mbunge
lakini akihama Chama atapoteza
Ubunge wake.

Inapendekezwa ukomo wa
Ubunge uwe vipindi vitatu vya
miaka mitano mitano. Hata hivyo,
wananchi wanaweza kumwondoa
mbunge wao kabla ya mwisho wa
kipindi chake.

Inapendekezwa pia kusiwepo na
uchaguzi mdogo isipokuwa kama
nafasi inayokuwa wazi inatokana
na Mbunge huru ndipo
utafanyika uchaguzi mdogo
kujaza nafasi hiyo, lakini kama
nafasi ikiwa wazi kutokana na
Mbunge wa Chama cha Siasa basi
nafasi hiyo, ijazwe na mtu kutoka
Chama hicho.

Inapendekezwa Spika na Naibu
Spika wasitokane na Wabunge na
wasiwe Viongozi wa vyama vya
Siasa.

TUME YA UCHAGUZI

Tume imefanya uchambuzi wa
maoni ya wananchi kuhusu Tume
ya Uchaguzi. Tume inapendekeza
jina la tume liwe Tume Huru ya
Uchaguzi.

Tume pia
inapendekeza sifa za wajumbe wa
Tume Huru ya Uchaguzi ziwekwe
kwenye Katiba. Wajumbe wa
Tume Huru ya Uchaguzi
watapatikana kutoka miongoni
mwa watu wenye sifa
zilizoainishwa ndani ya Katiba
kwa kuomba. Majina ya
waombaji yatachambuliwa na
Kamati ya Uteuzi ambayo
Mwenyekiti wake atakuwa Jaji
Mkuu na wajumbe wengine sita
ambao ni Majaji Wakuu wa nchi
Washirika, Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano, Maspika
wa Mabunge wa nchi Washirika
na Mwenyekiti wa Tume ya Haki
za Binadamu.

Kamati ya uteuzi itapendekeza
majina ya watu wanaofaa kwa
Rais ambaye atateua Mwenyekiti,
Makamu Mwenyekiti na
Wajumbe wengine. Bunge
litathibitisha uteuzi wao.

Wabunge na viongozi wa aina
hiyo hawatakuwa na sifa za kuwa
wajumbe wa tume ya uchaguzi.

Inapendekezwa Tume huru ya
Uchaguzi isimamie masuala ya
uchaguzi, kura ya maoni na
Usajili wa Vyama vya Siasa.

MAHAKAMA

Kuhusu Mahakama
inapendekezwa kuanzishwa kwa
Mahakama ya Juu (Supreme
Court) Majaji wa Mahakama ya
Juu na Mahakama ya Rufani
watateuliwa na Rais baada ya
kupendekezwa na Tume ya
Utumishi wa Mahakama.

MUUNDO WA MUUNGANO

Ndugu Wananchi,
Suala la muundo wa Muungano
ndilo lililokuwa gumu kuliko
masuala yote. Tume ilitumia
muda mwingi kuchambua maoni
ya wananchi.

Pamoja na kwamba
hadidu za rejea zilielekeza Tume
kuzingatia uwepo wa Muungano,
baadhi ya wananchi walitoa
maoni kwamba Muungano
uvunjwe na Tume iliyapokea
maoni hayo. Licha ya kwamba
waliotaka kuvunjwa muungano
walikuwa wachache sana, Tume
ilichambua sababu walizotoa na
kuridhika kwamba hazikuwa na
uzito.

Wananchi walio wengi walitaka
Muungano uendelee. Kati yao
wapo waliopendekeza Muungano
wa Serikali moja, Serikali mbili,
Serikali tatu, Serikali nne na
muungano wa mkataba.

Sababu
za wale waliopendekeza Serikali
nne hazikuwa na uzito, kwa hiyo
Tume ikaamua kutopendekeza
muundo huo.

Wananchi waliopendekeza
Serikali moja walikuwa wachache
lakini sababu zao zilkuwa na
uzito. Hata hivyo, Tume kwa
kuzingatia hali halisi iliona ni
changamoto kubwa kuwa na
Muungano wa Serikali Moja.

Wananchi waliopendekeza
Muungano wa Mkataba walikuwa
wengi (hasa wananchi wa
Zanzibar) na sababu zao zilikuwa
na uzito. Lakini uchambuzi wa
Tume ilionekana wazi kwamba ili
kupata mkataba lazima kwanza
kuwe na nchi mbili huru kabisa
lakini hakukuwa na mazingira ya
uhakika ya kupata mkataba wa
muungano. Tume iliona kuna
changamoto ya muungano
kuvunjika ingawa waliotoa maoni
walisisitiza muungano ubaki.

Hivyo, Tume iliamua
kutopendekeza muundo huo.

Wananchi waliopendekeza
Tanzania iendelee na Muundo wa
sasa wa Serikali mbili walikuwa
wengi na sababu zao zilikuwa
nzito. Hata hivyo, wananchi
katika kundi hili walipendekeza
mabadiliko mengi na makubwa.

Tathmini ya Tume ilionyesha
kwamba isingewezekana kufanya
mabadiliko yote
yaliyopendekezwa.

Wananchi waliopendekeza
muundo wa Serikali tatu
walikuwa wengi kuliko makundi
yote. Sababu zao zilikuwa nzito
lakini pia kulikuwa na
changamoto nyingi na nzito.

Pamoja na maoni ya wananchi
Tume ilirejea sababu za
kupendekeza muundo huu
zilizotolewa na Tume zilizopita na
Tafiti zilizofanywa na Tume
kuhusu aina mbalimbali za
Muungano. Baada ya yote hayo
Tume ilifikia uamuzi wa
kupendekeza mfumo wa Serikali
tatu. Yaani Serikali ya Shirikisho,
Serikali ya Tanzania Bara na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

ORODHA YA MAMBO YA
MUUNGANO

Ndugu Wananchi,
Tume imependekeza katika
Rasimu ya Katiba kuwa orodha ya
Mambo ya Muungano yawe 7
badala ya 22 yaliyopo sasa.

Mambo ya muungano
yanayopendekwa ni:

1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania
2. Ulinzi na Usalama wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania
3. Uraia na Uhamiaji
4. Sarafu na Benki Kuu
5. Mambo ya Nje
6. Usajili wa Vyama vya Siasa
7. Ushuru wa bidhaa na mapato
yasiyo ya Kodi yatokanayo na
Mambo ya Muungano.

BENKI KUU

Kwa kuwa Tume imependekeza
Muungano wa Shirikisho
kutokana na uzito wa maoni ya
wananchi. Hivyokutakuwa na
Benki Kuu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
itakayokuwa na wajibu wa
kusimamia masuala ya Sarafu na
Fedha za Kigeni na Benki za
Washirika wa Muungano.

BENKI ZA SERIKALI ZA
WASHIRIKA

Kutokana na pendekezo la
kuwepo kwa Serikali ya
Shirikisho la Nchi tatu,
inapendekezwa kuwepo kwa
Benki zitakazokuwa na jukumu la
kutunza akaunti ya fedha za
Serikali za kila Mshirika wa
Muungano na kuzisimamia benki
za biashara katika mamlaka zao.

BAADHI YA MAMBO AMBAYO
HAYAMO KWENYE RASIMU YA
KATIBA

Serikali ya Majimbo
Ndugu Wananchi,

Tume ilipokea maoni kuhusu
mambo mengine muhimu
ambayo hayamo katika rasimu
hii. Moja ya mambo hayo ni
Serikali za Majimbo. Tume
ilichambua maoni na sababu za
wananchi kupendekeza Serikali
za Majimbo lakini Tume ilibaini
changamoto nyingi na ikaamua
kutopendekeza muundo huu.

Kwanza, baada ya kuamua
kupendekeza Muundo wa
Muungano wa Serikali Tatu,
ilionekana ni dhahiri kuongeza
ngazi nyingine ya Serikali
ingeleta gharama kubwa. Serikali
nyingine kumi zingekuwa na
Wakuu wa Majimbo, Mabaraza ya
Mawaziri na Mabunge na
gharama yake ingekuwa kubwa.

Pili, katika kutembelea nchi
Tume ilishuhudia dalili za wazi za
mivutano ya Udini,
ukanda,malalamiko ya
upendeleo wa baadhi ya maeneo
na ukabila. Dalili zilikuwa wazi
kwamba utawala wa majimbo
ungeirudisha nchi kwenye
utawala utakaoigawa nchi kwa
misingi ya ukabila, udini na
ukanda na kuzigawa rasilimali za
taifa kikanda na hivyo kuleta
tofauti kubwa ya kimaendeleo
katika nchi.

Mahakama ya Kadhi

Ndugu wananchi,
Jambo la pili ni mahakama ya
kadhi. Tume ilipokea maoni
mengi kuhusu suala hili.

Baadhi
ya wananchi walitaka mahakama
ya kadhi iingizwe kwenye Katiba
na wengine walipinga.

Baada ya
kuamua kuwa Muundo wa
Muungano uwe wa Serikali Tatu,
Tume iliona kuwa Mahakama ya
Kadhi siyo suala la Muungano na
imeliacha ili lishughulikiwe na
Washirika wa Muungano.
Hata hivyo ilionekana kuwa suala
siyo kuwapo au kutokuwapo kwa
mahakama ya kadhi. Mahakama
hizo zinaweza kuwapo bila ya
kuwa katika Katiba.

Zanzibar
kuna mahakama ya kadhi bila
kuingizwa kwenye Katiba ya
Zanzibar. Kwa kutumia uzoefu
huo hata Tanzania Bara inaweza
kupata ufumbuzi wa suala hili.

Wakuu wa Mikoa na Wakuu
wa Wilaya

Jambo la Tatu ni Kuwepo au
kutokuwepo kwa Wakuu wa
Mikoa na Wilaya. Baadhi ya
Wananchi walitaka Wakuu wa
Mikoa na Wilaya wasiwepo,
wengine walitaka Wakuu wa
Mikoa na Wilaya waendelee
kuwepo lakini wachaguliwe na
wananchi na waengine wakasema
wawepo na waendelee kuteuliwa
na Rais kama ilivyo sasa. Tume
ilitafakari kuhusu suala hili na
kuamua kwamba siyo suala la
Muungano na kwa kuwa Muundo
wa Muungano imependekezwa
uwe wa Serikali Tatu, Tume iliona
suala la uwepo au kutokuwepo
na namna ya upatikanaji wa
Wakuu wa Mikoa na Wilaya
lishughulikiwe na Washirika wa
Muungano.

Serikali za Mitaa
Kuhusu Serikali za Mitaa, Tume
ilipokea maoni kutoka kwa
wananchi kuhusu kuziimarisha
Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa
kuzipatia uhuru kamili wa
kujiamulia mambo yao bila
kuingiliwa na Serikali Kuu.

Tume
ilitafakari suala hili na kuamua
kwamba siyo jambo la Muungano
na hivyo, litashughulikiwa
kwenye Katiba za Washirika wa
Muungano.

Uraia wa Nchi mbili
Ndugu Wananchi,
Jambo la tatu ni Uraia wa Nchi
mbili. Tume ilipokea maoni
kutoka kwa wananchi mbalimbali
kuhusu kuwekwa kwenye Katiba
suala la Uraia wa nchi mbili.

Baada ya kufanya uchambuzi kwa
kutengenisha mambo yapi ni ya
Kikatiba na yapi yanaweza
kutekelezwa bila kuingizwa
kwenye Katiba bali kwenye
Sheria inayohusu jambo husika,

Tume imependekeza kuwa suala
la Uraia wa nchi mbili linaweza
kuwekwa kwenye Sheria badala
ya kuwekwa kwenye Katiba. hii
ni kwa sababu kutokana na utafiti
uliofanywa na Tume, suala hilo
linaweza kubadilika wakati
wowote na hivyo likiwa kwenye
Katiba linaweza kuifanya Katiba
kubadilishwa mara kwa mara.

MWISHO

Naomba nichukue fursa hii kwa
niaba ya Tume kuwashukuru
Watanzania wote kwa kushiriki
kikamilifu katika mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba, kuanzia
hatua ya kutoa maoni na
kuwachagua wawakilishi wenu
watakaopata fursa ya kuipitia,
kuijadili na kuitolea maoni
Rasimu ya Katiba.

Ushirikiano
huu ulikuwa muhimu sana kwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba
hasa ukizingatia kuwa lengo ni
kupata Katiba Mpya ambayo
itaakisi ndoto na matakwa ya
Wananchi wa Tanzania.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
inatoa shukrani za dhati kwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar:

1. Kwa kuipatia vifaa afisi na
mahitaji ya lazima
2. Kwa kuiwezesha Tume
kutekeleza majukumu yake
kwa ukamilifu,
3. Kwa kutokuingilia Uhuru wa
Tume wakati wa Utekelezaji
wa Majukumu yake na
4. Kutoa Wataalam wenye
Weledi, Mahiri, Makini na
Waadilifu ambao wameunda
Sekretarieti ya Tume.

Ndugu Wananchi,
Shukrani za pekee ziwaendee:
1. Wakuu wa Mikoa,
2. Wakuu wa Wilaya,
3. Wakurugenzi / Makatibu wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa,
4. Makamanda wa Polisi wa
Mikoa na Wilaya,
5. Watendaji wa Kata, Vijiji,
Mitaa na Masheha.
Kwa kuisaidia Tume kutekeleza
Majukumu yake kwa ufanisi.

Aidha, tunazishukuru Asasi za
Kiraia, Taasisi, Jumuiya za Kidini,
Vyama vya Siasa na Makundi
mbalimbali kwa namna
walivyoshiriki katika
kuhamasisha wananchi kushiriki
katika kutoa maoni.

Mwisho ingawa siyo kwa
umuhimu, Tunawashukuru
Wanahabari wote kwa kazi nzuri
waliyoifanya ya kuisaidia Tume
kufikisha taarifa mbalimbali za
Tume kwa Wananchi na katika
kuhamasisha Wananchi kushiriki
katika mchakato wa Mabadiliko
ya Katiba.

Nachukua nafasi hii kuwaomba
Wananchi kupitia Mabaraza ya
Katiba ya Wilaya, Mabaraza ya
Katiba ya Asasi, Taasisi na
Makundi ya Watu wenye
Malengo yanyofanana kushiriki
vyema, kwa umakini, utulivu na
kwa amani katika hatua hii ya
kuipitia, kuijadili na kuitolea
maoni Rasimu ya Katiba.
Tume imekuwa ikithamini na
itandelea kuthamini mawazo na
maoni kutoka kwa Watanzania
wote.

Rasimu ya Katiba itapatikana
kwenye tovuti ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ya
www.katiba.go.tz