Mbunge Mtwara Adakwa na Polisi kwa Uchochezi.

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemkamata
mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji
likimtuhumu kuchochea vurugu za kupinga
mradi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo
kwenda jijini Dar es Salaam.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na
Msemaji wa Jeshi la polisi nchini, Advera Senso
zinaeleza kuwa Murji alikamatwa jana jioni
nyumbani kwake maeneo ya Shangani mjini
Mtwara.

Kukamatwa kwa mbunge huyo kunakuja ikiwa
zimepita siku tano tangu viongozi wanne wa
vyama vya upinzani mkoani Mtwara,
kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mtwara, Juni 4, mwaka huu wakikabiliwa na
mashtaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya
uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Washtakiwa hao ni Katani Ahmed Katani (33)
na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35)
wa NCCR Mageuzi na Hamza Licheta (51) wa
TLP, wote wakazi wa Mtwara.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa baada ya polisi
kumkamata mbunge huyo, walifanya upekuzi
katika nyumba yake kwa saa kadhaa na baada
ya kujiridhisha walikwenda kupekua na ofisi
yake.

"Amekamatwa kwenye saa 11:00 jioni, hata
hati ya kukamatwa kwake imeeleza kuwa
anatuhumiwa kuchochea vurugu za
kupinga gesi inayopatikana mkoani Mtwara
kwenda Dar es Salaam," alisema Katibu wa
Mbunge huyo, Meckland Millanzi.

Katika ufafanuzi wake Senso alisema
kukamatwa kwa mbunge huyo ni jambo la
kawaida na kwamba hivi sasa unaandaliwa
utaratibu ili faili lake lipelekwe kwa
Mwanasheria wa Serikali.

"Acheni polisi ifanye kazi yake kama
kutakuwa na la ziada tutawaeleza ila kwa
sasa tunaandaa utaratibu wa suala hili
kwenda kwa mwanasheria wa Serikali,"
alisema Senso.

Murji amekamatwa ikiwa zimepita siku 16
tangu kutokea vurugu kubwa mkoani Mtwara
zilizodumu kwa siku mbili, ambapo polisi
walipambana na makundi ya vijana
wanaopinga mradi wa bomba la gesi kujengwa.

Vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya watu
kupoteza maisha huku wengine wakiachwa
majeruhi na mali nyingi kuharibiwa, ziliibuka
baada ya hotuba ya bajeti ya wizara ya nishati
na madini kusomwa bungeni.

Mvutano kuhusu mradi wa bomba la gesi
ulianza Novemba 16, mwaka jana baada ya
Serikali kutuma kamati inayoratibu maoni ya
sera ya gesi "The Natural Gas Policy of Tanzania
-2013" ambayo ilifika mkoani Mtwara
kukusanya maoni ya wananchi.

Katika mikutano yake mjini Mtwara, wananchi
wengi hawakukubaliana na wazo la
kusafirishwa gesi nje ya Mtwara kwa njia ya
bomba.

Hali hiyo ndiyo iliyowasukuma
viongozi wa vyama kuhamasisha wananchi
kuhusu suala hilo.