Nelson "Madiba" Mandela Aendelea Vizuri

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
amesema kuwa afya ya rais wa
zamani wa taifa hilo Nelson
Mandela imeanza kuimarika
kidogo kutokana na matibabu
anayopewa na Madaktari wake
jijini Pretoria.

Zuma amewaambia wabunge kuwa
Mandela anayefahamika kwa jina
maarufu kama Madiba ameanza
kuimarika na ni habari njema kwa
raia wa nchi hiyo ambao
wamekuwa wakikumbwa na
wasiwasi kutokana na afya yake
kuendelea kudorora.

Rais huyo ameongeza kuwa kila
mmoja anakumbuka mchango wa
Mandela ambaye alifungwa jela
miaka 27 akiwa katika harakati za
kupinga ubaguzi wa rangi nchini
humo na baadaye kufanikiwa
kuwa kiongozi wa kwanza mweusi
nchini humo mwaka 1994.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini
amewataka raia wa nchi hiyo na
dunia nzima kuendelea
kumwombea Mandela ili apate
nafuu haraka na kuruhisiwa
kurudi nyumbani.

Familia ya Mandela imesema kuwa
imeguswa mno na salamu za heri
njema zinazotumwa na watu
mbalimbali duniani kumtakia
kiongozi huyo wa zamani nafuu ya
haraka.

Mandela mwenye umri wa miaka
94 alilazwa hospitalini Jumamosi
iliyopita baada ya kuanza
kusumbuliwa na mapafu tatizo
ambalo limemsumbua kwa muda
mrefu.

Hii ni mara ya nne kuanzia mwezi
Desemba mwaka uliopita kwa
Mandela ambaye atatimiza miaka
95 mwezi ujao kulazwa hospitalini
na mara ya mwisho ilikuwa mwezi
Aprili mwaka huu.

Mara ya mwisho kwa Mandela
kuonekana hadharini ilikuwa
mwezi Julai mwaka 2010 wakati
wa ufunguzi wa mashindano ya
soka ya kombe la dunia nchini
humo.