Miaka 67 Jela Kwa Ujambazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi
Moshi, mkoani Kilimanjaro
imewahukumu raia wawili wa
Kenya na mwanamke mmoja
Mtanzania jela miaka 67 baada
ya kupatikana na hatia ya kula
njama na kupora Sh milioni
239 kutoka benki ya NMB tawi
la Mwanga, Kilimanjaro.

Uporaji huo ulifanyika Julai
11,2007 ambapo pia watu hao
waliiba bunduki aina ya Sub
Machine Gun (SMG) mali ya
Jeshi la Polisi nchini, na
kumuua askari Polisi Michael
Milanzi aliyekuwa lindo.
Watuhumiwa hao waliofungwa
ni Samweli Gitau maarufu kwa
jina la Saitoti na Michael
Joseph Kimani (wote kutoka
Kenya) na Mtanzania Elizabeth
Elias maarufu kwa jina la Bella
mkazi wa Kwangulelo mkoani
Arusha.

Jopo la makakimu watatu
wakiongozwa na Panterine
Kente liliwahukumu kwenda
jela miaka saba kwa kosa la
kwanza ambalo ni kula njama;
miaka 30 kila mmoja kwa kosa
la uporaji pamoja na miaka 30
kwa kosa la wizi wa silaha.

Hakimu huyo alisema kuwa
adhabu hizo zinaenda pamoja
hivyo washitakiwa
watatumikia kifungo cha
miaka 67 jela, mbali na
hukumu hiyo Mahakama hiyo
pia iliwaachia huru ndugu
watatu ni ambao ni Devotha
Elias Masenza, Ntibasana Elias
Masenza na Julian Elias
Masenza na mtu mwingine
Calist Kanje baada ya ushahidi
dhidi yao kushindwa
kuishawishi Mahakama.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo ,
wakili wa Serikali Tamali
Mndeme aliomba Mahakama
kutoa adhabu kali kwa
washitakiwa ili iwe fundisho
kwa watu wengine wenye nia
ya kutenda makosa kama
hayo.

Chanzo:Habarileo