Mizengo Pinda atoe kauli tete Bungeni wiki iliyopita ya
kulichochea Jeshi la Polisi liendeleze vipigo na mateso kwa wananchi
aliodai wanakaidi sheria za nchi, wamejitokeza baadhi ya watu, wakiwamo
mawaziri wakijaribu kuipaka sukari kauli hiyo ili itafsiriwe na
kuonekana kama ni ya kuhimiza utiifu wa sheria.
Hatari ya kauli hiyo kwa amani na usalama wa
wananchi inatokana na ukweli kwamba inaonyesha kama vile nchi yetu
inatawaliwa kijeshi. Kinyume chake, nchi yetu inaongozwa na Katiba, kwa
maana kwamba Serikali iliyopo madarakani ilichaguliwa na wananchi
kupitia sanduku la kura. Haikupatikana kwa mtutu wa bunduki na mapinduzi
ya kijeshi.
Kwa maana hiyo, Katiba ya Tanzania na sheria
zilizotungwa na Bunge ni mwongozo kwa watawala kuhusu namna ya kuendesha
Serikali kwa njia za kidemokrasia na kuhakikisha usalama wa raia na
mali zao. Anapotokea kiongozi wa juu wa Serikali akalichochea Jeshi la
Polisi kuvunja Katiba na sheria za nchi kwa kufanya vitendo
vinavyosababisha hofu na kuhatarisha amani na maisha ya raia lazima
wananchi wapaze sauti, wamlaani kwa nguvu zote na wamwambie ‘hapana’.
Kauli ya Waziri Mkuu Pinda inatia hofu, hasa
inapotolewa kwa Jeshi la Polisi lenye muundo uliorithiwa kutoka kwa
wakoloni. Tofauti na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo mwaka
1964 lilifanyiwa mabadiliko makubwa kutoka jeshi la kikoloni na kuwa
jeshi la wananchi, Jeshi la Polisi tulilorithi kutoka kwa wakoloni
lilibakia hilohilo kimuundo na kwa kiasi kikubwa kisera.
Kimsingi ni Jeshi lililoundwa kupokea amri na
kutekeleza matakwa ya watawala ya kuwakandamiza wazalendo, hata kama
wazalendo hao wanadai haki zao za kiraia na kikatiba kama Jeshi la
Polisi la Makaburu wa Afrika Kusini lilivyokuwa likiwaua na kuwatesa
wazalendo waliokuwa wakipinga ubaguzi wa rangi. Ndiyo maana hapa nchini
umekuwapo uhasama mkubwa kati ya jeshi hilo na wananchi. Watawala
wanaonekana kufurahia hali hiyo ambayo tayari imesababisha vifo na
mateso kwa raia wasiokuwa na hatia.
Waziri Mkuu anasema jeshi hilo lazima liwapige
wananchi anaodai wanakaidi amri halali ya Polisi. Tunauliza amri halali
ya Polisi ni ipi? Kupiga marufuku mikutano ya vyama vya upinzani na
kuisambaratisha kwa mabomu na silaha za kivita bila sababu za msingi ni
amri halali ya wapi? Tunasema hiyo siyo amri halali na inakwenda kinyume
na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inayovitaka vyama hivyo
kutoa tu taarifa ya mikutano hiyo kwa Polisi ndani ya saa 24 ili
vipatiwe ulinzi. Jeshi hilo sasa limejipachika madaraka ya kutoa vibali,
kukataa ama kukubali kwa kutoa masharti ya ajabu. Je, hayo ni maagizo
ya chama tawala na serikali yake?
Sisi tunasema kauli ya Waziri Mkuu Pinda inahitaji
mjadala wa kitaifa. Ni kauli hatari. Tuikatae, kwani inalenga
kuhatarisha amani na umoja wetu. Jaji mstaafu Mark Bomani juzi
alionyesha njia alipotahadharisha Serikali na jeshi hilo dhidi ya
kutumia nguvu kubwa kukabiliana na umma kwa kutumia silaha za moto.
Alionyesha wasiwasi kama kweli Polisi wana uelewa mzuri wa sheria kuhusu
matumizi ya silaha za moto au wanafanya kazi kwa kuagizwa tu.
Tunahitaji sauti nyingi kama hiyo.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi