Uingereza Kuwafidia Mau Mau

Serikali ya Uingereza inatarajiwa
kuomba msamaha pamoja na
kuwalipa fidia manusura wa harakati
za ukombozi wa Uhuru wa Kenya
Mau Mau.

Waliokuwa wanachama wa vuguvugu
hilo waliwasilisha kesi mahakamani
kwa mateso na dhuluma walizodai
kutendewa na uliokuwa utawala wa
ukoloni miaka ya 50.

Waziri wa mambo ya nje wa
Uingereza William Hague, anatarajiwa
kutangaza kiwango cha pesa ambazo
serikali ya Uingereza iko tayari kutoa
kama fidia, duru zikisema kuwa
huenda ikawa dola milioni 20
Zaidi ya wakenya 5,000, waliteswa
baadhi wakinyanyaswa na waliokuwa
wakoloni wa Uingereza.

Uingereza ilipigana vita vikali dhidi ya
Mau Mau, waliokuwa wanadai ardhi
na kuondoka kwa utawala wa kikoloni.
Manusura wa vita hivyo wamekuwa
wakiidai Uingereza kuwalipa fidia kwa
miaka mingi.

BBC ina habari kuwa bwana Hague
atawaomba radhi waathiriwa wa vita
vya Mau Mau, wakati akitangaza
kiwango cha pesa watakazotoa kama
fidia kwao.

Serikali ya Uingereza awali ilikuwa
imesema kuwa madai yote ya vitedno
walivyofanya wakoloni ni juu ya
serikali ya Kenya tangu kuipa uhuru
mwaka 1963 na kuwa kwa sasa
haiwezi kutakiwa kulipa.

Lakini mwaka 2011, mahakama
iliamuru kuwa, wanaodai fidia, Paulo
Muoka Nzili, Wambuga Wa Nyingi na
Jane Muthoni Mara, walikuwa na haki
ya kudai fidia kutoka kwa Uingereza .

Mawakili wao wanasema kuwa Nzili
alihasiwa , huku Bwana Nyingi
akichapwa vibaya wakati Bi Mara
akiteswa kimapenzi katika kambi za
mateso ambako waliokuwa
wanapinga ukoloni walikuwa
wakifungwa.

Baada ya uamuzi wa kesi hiyo,
ilirejeshwa katika mahakama kuu ili
kuamua pesa watakazolipwa na ofisi
ya jumuiya ya madola.

Duru zinasema kuwa serikali
ilikumbwa na wakati mgumu kupata
mashahidi na stakabadhi muhimu
kuweza kuelezea ukweli katika kesi
hiyo.

Lakini Oktoba mwaka jana, mahakama
iliamua kuwa waathiriwa
waliowasilisha kesi hiyo mahakamani
walikuwa na haki ya kufidiwa kwani
walikuwa na kesi nzito dhidi ya serikali
ya Uingereza.

Watatu hao walikuwa wamesema
kuwa wangekubali wahusika wa kesi
kuafikiana nje ya mahakama lakini pia
walikuwa wanataka kufuata sheria
kwani waliona wangepata haki katika
mahakama.


Kutoka:BBC