Mchina Agongwa na Gari na Kufariki

RAIA wa China aliyetambuliwa kwa jina la Ruo Yaowu (34) amekufa papo
hapo baada ya kugongwa na gari wakati akivuka barabara.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela
alithibitisha hayo jana na kusema kuwa, ajali hiyo ilitokea juzi saa
7:00 usiku katika barabara ya Bagamoyo eneo la Boko, Kinondoni.

Alisema gari namba T865 AHB aina ya Toyota Canter, likiendeshwa na mtu
asiyefahamika akitokea Bunju kwenda Tegeta, alimgonga mtu huyo ambaye
alikufa papo hapo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili na msako wa kumtafuta dereva aliyekimbia baada ya
ajali unaendelea.

Katika tukio jingine, maiti moja ya mwanaume aliyetambuliwa kwa jina
moja la Chalii anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 15 ba 20,
imekutwa ikiwa imelala pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi alisema tukio
hilo ni la juzi saa 4:10 usiku katika eneo la Ferry, wilaya ya Ilala.

Maiti hiyo ilikutwa ikiwa pembezoni huku ikiwa haina jeraha lolote
isipokuwa ilikuwa inatoka damu mdomoni na puani. Chanzo cha kifo chake
hakijafahamika na maiti imehifadhiwa hospitali ya Taifa Muhimbili.