Azikwa Akiwa Hai

Mbeya. Msaidizi wa zamani wa Padri (Katekisita) katika Kigango cha
Kanisa Katoliki Kijiji cha Mkwajuni, Florian Mwamosi (70) amekufa
baada ya kuzikwa akiwa hai katika kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua
kwa njia ya kishirikina.
Tukio hilo limetokea katika Kitongoji cha Maweni kijijini hapo
wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani alikiri kutokea kwa
tukio hilo akieleza kuwa lilitokea saa 9:00 mchana katika kijiji
hicho cha Maweni Mkwajuni wilayani Chunya.

"Marehemu aliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na mawe
kwa tuhuma za kuhusika na uchawi na kusababisha kifo cha Peter
Robert," alisema.

Kamanda Athumani alisema kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo
unaendelea na kwamba wahusika wote wa tukio hilo wamekimbia na
kuzihamanyumba zao, hivyo polisi wanaendelea na msako wa kuwatia
mbaroni watuhumiwa na kwamba tayari kaburi hilo limefukuliwa jana
kutenganisha maiti hizo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa marehemu huyo ambaye alikuwa
akituhumiwa kwa ushirikina aliwahi kuwa Katekista wa kigango hicho
hadi mwaka 2007.

Wameeleza kuwa Mwamosi alikwenda kuhudhuria mazishi ya Peter Robert
(28) katika kitongoji hicho cha Maweni, baada ya kufuatwa nyumbani
kwake na watu wakitaka aende kwa sababu yeye ni mmoja wa wazee wa mila
katika kitongoji hicho.

"Bwana Mwamosi alikuwa akituhumiwa kwa uchawi kwa muda mrefu na wenzie
wawili, hivyo alipofika makaburini ilianza minong`ono ya watu na huku
wengine wakiguna na ndipo alipoombwa aingie kaburini kwa ajili ya
kupokea jeneza lililobeba mwili wa marehemu Peter Robert," alisema
mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph.

Alisema kuwa baada ya kuingia kaburini akiwa na watu wengine watatu
wenzake walitoka kwa haraka na kumwacha Mwamosi peke yake ndipo kundi
la watu waliokuwa eneo hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa
kumpiga mawe huku wakimwamuru akae chini.

Shuhuda huyo alisema kuwa baada ya kukubali kukaa chini akiwa ndani ya
kaburi hilo, walianza kumfukia naalipofukiwa nusu ya mwili wake
waliingiza jeneza la marehemu Peter na kuliweka juu yake na kuanza
kulifukia kaburi hilo.

"Baada ya kukaa chini ndani ya kaburi hilo ndipo walianza kumfukia kwa
udongo na baadaye wakachukua jeneza la marehemu na kuliweka juu yake,
kisha kumfukia na udongo na taratibu za mazishi ziliendelea kwa ajili
ya marehemu Peter,"alisema.

Alidokeza kuwa chanzo cha tukio hilo ni marehemu Robert kuugua ghafla
tumbo, ndipo ndugu zake walipoamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kwa
ajili ya kupata matibabu na baada ya siku tatu alifariki dunia.

Kamanda huyo amewasihi wakazi wa Mkoa wa Mbeya kuacha tabia kama hizo
kwani kufanya hivyo ni kuuchafua mkoa na kuwa na sifa mbaya, hivyo
kusababisha maendeleo ya mkoa kurudi nyuma.
Januari 12, mwaka huu wakazi wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya
Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya walikufa baada ya kufukiwa wakiwa
hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio
linalohusishwa na imani za kishirikina.

Chanzo:Mwananchi