Serikali Yagomea Ushauri Wa Wabunge

Serikali imekataa ushauri wa wabunge na kusema kuwa itaendelea
kuwaajiri wastaafu mbalimbali nchini hadi hapo soko la ajira
litakapojitosheleza.
Mbali na hilo, jana Serikali ilitangaza bungeni kuwa kazi za wakuu wa
mikoa siyo ajira rasmi, bali ni ajira za kisiasa ambazo hazipaswi
kuhesabiwa.
Akijibu swali bungeni jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti
ya Utumishi wa Umma) Celina Kombani, alikiri kuwa bado Serikali
inaendelea kutoa ajira kwa watu ambao wamestaafu na kuwa itaendelea
kufanya hivyo kwa siku za usoni.
Alikuwa akijibu swali la Vicent Nyerere (Musoma-Chadema) ambaye
alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kusitisha kutoa mikataba kwa
wastaafu ili wahitimu wanaotoka vyuoni wapate ajira na kujenga nchi
yao.
Mbunge huyo pia alihoji nafasi za wakuu wa mikoa nchini ambao wengi
hufanya kazi wakiwa katika umri mkubwa, huku baadhi wakiwa wamestaafu
utumishi wa umma. Waziri alisema ni kweli kuwa wako wataalamu wengi
wanaohitimu vyuo vikuu hapa nchiniambao wanahitaji kuingia katika soko
la ajira, lakini hupatiwa ajira kulingana na uwezo na bajeti ya
Serikali.
Kuhusu wastaafu kuendelea kupewa ajira, alisema "Hilo linatokana na
utaalamu walionao ambao ni vigumu kuziba nafasi zao kwa kipindi cha
haraka."
Kombani alizitaja kada ambazo Serikali inatoa mikataba kwa wastaafu
kuwa ni walimu, waganga, wahandisi na wahadhiri wa vyuo ambao alisema
nafasi zao ni adimu.



Chanzo:Mwananchi.co.tz