Vurugu zazuka Liwale Na Arusha

Liwale/Arusha. Uharibifu mkubwa wa mali ulifanywa juzi usiku Mjini
Liwale, Lindi baada ya wananchi wenyehasira kuchoma moto nyumba za
viongozi waandamizi, makao makuu ya Halmashauri ya Wilayana maghala ya
mazao kutokana na kuchukizwa kushushwa kwa bei ya korosho.
Nyumba zilizochomwa moto ni za Mbunge wa Liwale (CCM), Faith Mtambo,
Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja, Hassan Myao na Makamu wake,
Hassan Mpako, Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Liwale,Amina Mnocha,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Abbas Chigogola ambaye
pia ng'ombe wake tisa walikatwakatwa mapanga na kuachiwa ndama watatu.
Nyingine ni nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Liwale, Mohamed
Ng'omambo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Lindi, Mwenyekiti wa Chama
cha Msingi Minali, Mohamed Limbwilindi na Katibu wa chama hicho, Juma
Majivuno.
Wakati hayo yakitokea Lindi, huko Arusha, vurugu kubwa za wanafunzi wa
Chuo cha Uhasibu zilizuka jana baada ya kuuawa kwa mwanafunzi Henry
Kago (22), juzi usiku.
Kago, ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili,anadaiwa kuwa
alifariki juzi saa nne usiku baada ya kuchomwa kisu na watu
wasiojulikana, akiwa njiani eneo la Kanisa la Wasabato akitokea chuoni
hapo kujisomea.
Ghasia za Liwale
Ghasia hizo zilianza juzi mchana katika Kijiji cha Liwale B na
ziliendelea usiku kucha hadi jana asubuhi.
Watu walioshuhudia ghasia hizo walisema chanzo ni wakulima kudai
kulipwa Sh600 na siyo Sh200 za mauzo ya korosho kwenye Chama cha
Msingi Minali.
Bei ya kilo moja ya korosho waliyokubaliana wakulimana chama hicho ni
Sh1,200 na mara ya kwanza kiliwalipa Sh600 kwa kilo na kuahidi kulipa
nusu nyingine baadaye.
Hata hivyo, viongozi wa Ushirika walibadili uamuzi na kulipa Sh200 kwa
maelezo kuwa mauzo hayakuwa mazuri kitendo ambacho kiliwakasirisha
wakulima haoambao waligoma kupokea fedha hizo.
Baadaye ilielezwa kuwa viongozi wa Minali walipeleka fedha hizo polisi
ili malipo yafanyike huko, lakini ghasia zikaibuka na wakaamua
kusitisha malipo hayo na ndipo wananchi wakaamua kuingia mitaani.
Mmoja wa mashuhuda alisema "Polisi walijaribu kuwadhibiti watu hao,
lakini walipoona wanazidiwa nguvu, wakawaachia wafanye wanavyotaka
ndiyo maana kumekuwa na uharibifu mkubwa."
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema kwa kifupi:
"Hali imetulia na vurugu zimemalizika lakini bado tuko kwenye kikao
kuzungumzia suala hili."
Wakulima hao walikerwa na tamko la Limbwilindi ambaye ndiye aliyetamka
kwamba watalipwa Sh200 kwa kilo na kuamua kwenda kuchoma moto nyumba
yake na baadaye ya Katibu wake Majivuno.
Limbwilindi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini, Majivuno
alipohojiwa alisema: "Tulikubaliana kuwalipa Sh1,200 kwa kila kilo,
lakini kwa awamu.
tuliwapa Sh600 awali na nusu yake imeshindikana kwakuwa mauzo hayakuwa
mazuri. Biashara haikwenda vizuri, ndiyo maana tukawaambia tutawalipa
Sh200 lakini wakakataa wanataka fedha zote Sh600, sasa sisihatuna
fedha hizo. Kama biashara ingefanyika kwa faida tungewalipa."
Habari zilizopatikana baadaye jana zilidai kuwa mke wa Mkungura, Amina
Mmoto amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale baada ya kupata
shinikizo la damu kutokana na sakata hilo.
Akizungumza kwa simu kuelekea Liwale, Mbunge Mtambo alisema:
"Nimesikitishwa na ghasia hizi... wamenitia hasara kubwa. Nyumba zangu
zote mbili zimechomwa, sijui nitaishi wapi. Hakuna kingine hizi
nisiasa tu...hakukuwa na sababu ya kufanya hivyo. Kama ni kulipwa
Sh200, mbona vyama vingine wamelipwa fedha hizo na hakukuwa na vurugu?
Jana kutwa nzima, Mji wa Liwale ulikuwa na utulivu huku polisi
wakitawanya makundi ya watu waliokuwa katika vikundi kwa mabomu ya
machozi na shughuli za biashara zilisimama na hakuna maduka wala
magenge yaliyofunguliwa.

Vurugu Arusha
Kutokana na vurugu hizo, Chuo cha Uhasibu cha Arusha, kimefungwa kwa
muda usiojulikana kwa usalama huku wanafunzi wakitakiwa kuondoka
chuoni hapo hadi watakapotangaziwa tena.
Licha ya kuelezwa kwamba aliuawa kwa kisu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Magesa Mulongo alisema taarifanyingine, zinaeleza kuwa aliuawa
akitokea katika Ukumbi wa Disko wa Bugaloo jirani na chuo hicho.
Baada ya taarifa za kifo hicho, wanafunzi wa chuo hicho walikusanyika
jana asubuhi na kuanza maandamano hadi Kituo Kikuu cha Polisi
wakilalamikia ulinzi duni.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alifika na kuwatuliza
wanafunzi hao na kuzungumza nao, kwa zaidi ya saa tatu wakati
wakimsubiri Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo, baada ya kufika chuoni hapo, mkuu huyo wa mkoa alishindwa
kuzungumza kutokana na kutokuwa na kipaza sauti na kusababisha
wanachuo kumzomea kabla ya uongozi wa chuo kubadili eneo la mkutano.
Hata hivyo, zomeazomea iliendelea na mkutano kuvunjika na FFU kufika
na kurusha mabomuya machozi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kumalizika kwa
Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama na uongozi wa chuo hicho, mkuu
huyo wamkoa alisema polisi wanafanya uchunguzi wa suala hilo.

"Baada ya kuletewa taarifa za tukio hili na Mbunge
Lema, niliondoka na kwenda kuwasikiliza wanachuo lakini tayari nilijua
mazingira yalikuwa yamebadilishwana pale nikagundua Lema ndiyo amekuwa
msemaji mkuu badala ya uongozi wa chuo au Serikali ya wanachuo. Ndiyo
maana mkaona na zomeazomea ile," alisema Mulongo.
Alimtuhumu mbunge huyo uchochezi na ameamuru kukamatwa kwake na
wanafunzi waliohusika na vurugu zile.

Lema alieleza kusikitishwa na agizo la kutakiwa kukamatwa akisema
alizuia maandamano kufika mjini...
"Nyie waandishi wa habari mlikuwepo nimezungumza zaidi ya saa mbili na
wale wanafunzi kuwasihi watulie wasiandamane na mimi ndiye nilimpigia
simu Mkuu wa Mkoa aje kuwasikiliza wanafunzi iweje niwachochee kufanya
fujo? Ninawasubiri waje wanikamate."


Chanzo: Mwananchi