Ahukumiwa Maisha Jela Kwa Kumbaka Mwanae

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi,
imemuhukumu Abisai Joseph (40) mkazi wa Mtaa wa Kigamboni, Kata ya
Shanwe mjini hapa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto
wake wa miaka sita.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya
wilaya hiyo, Chiganga Tengwa ambapo Joseph anadaiwa kutenda kosa hilo
Desemba 18 mwaka jana, saa tano usiku akiwa nyumbani kwake.
Awali, Mwendesha Mashtaka Ally Mbwijo, aliieleza mahakama kuwa siku
hiyo ya tukio Joseph alimbaka mwanaye baada ya kumvizia wakati alipo
toka kujisaidia haja ndogo.

Alidai kuwa baada ya kumkuta nje, alimvua nguo kisha alimweka sehemu
ya mapaja yake na kuanza kumfanyia kitendo hicho, na kwamba pamoja na
mtoto huyo kupiga kelele za kuomba msaada, mama yake aliyekuwa amelala
ndani hakuweza kusikia.

Mbwijo aliongeza kuwa baada ya kumaliza kufanyiwa kitendo hicho, mtoto
huyo aliingia ndani akilia, hali iliyomfanya mama yake amuulize,
lakini baba yake alijibu upesi kuwa alimkuta nje akibakwa na balozi
waowa nyumba kumi.
Alidai kuwa baada ya maelezo hayo, mama wa mtoto, Sauda Rajabu
alikwenda kwa majirani kuwapa taarifa ya kitendo hicho, lakini
walimshauri ende kutoa taarifa polisi.
"Akiwa hapo polisi mtoto huyo alikana kubakwa na balozi wao, bali
alisema aliyembaka ni baba yake mzazi," alidai.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne
akiwemo mtoto mwenyewe aliyebakwa na mshtakiwa hakuwa na shahidi
yeyote.

Hakimu Chiganga katika hukumu hiyo alisema mahakama imeridhika na
ushahidi uliotolewa na kwamba imemtia hatiani mshtakiwa kwa kuvunja
sheria namba 130 (1) (e) na 131 (3) kifungu cha marekebisho ya sheria
ya mwaka 2009.

Alisema kutokana na kosa hilo mahakama inamuhukumu Joseph kifungo cha
maisha jela ili liwe funzo kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.




Chanzo: Nassor Wazambi(fb)