Ubalozi Wa Ufaransa Washambuliwa

Bomu limelipuka nje ya ubalozi wa Ufaransa katika mji mkuu wa Libya,
Tripoli na kuwajeruhi walinzi wawili huku ikisababisha uharibifu
mkubwa.
Mlipuko huo ulisababisha uharibifu katika sehemu moja ya ofisi hizo na
pia kuharibu nyumba jirani.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli, Rana Jawad anasema kuwa inaaminika
kuwa mlipuko huo ulisababishwa na gari lililokuwa na mabomu.
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, aliitaka serikali ya Libya
kuchukua hatua za haraka kukabiliana na waliosababisha shambulio hilo.
Aliongeza kwamba shambulizi hilo lililenga nchi za kigeni
zinazopambana dhidi ya ugaidi.

Balozi za kigeni nchini Libya zimewahi kushambuliwa katika siku
zanyuma, lakini hili ndilo shambulizi la kwanza kubwa dhidi ya ubalozi
wa kigeni mjini Tripoli.

Shambulizi liliwahi kufanywa dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini
Benghazi mwezi Septemba mwaka jana na kusababisha kifo cha balozi
Christopher Stevens pamoja na maafisa wengine wamarekani.
Shambulio la leo lilifanyika muda mfupi baada ya saa kumi na
mojaasubuhi katika mtaa wa kifarahari mjini Tripoli.

Wakaazi wa eneo hilo walighadhabishwa sana na shambulizi hilo na
kulalamikia ukosefu wa ulinzi mzuri wa sehemu hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Libya, Mohammed Abdel Aziz alilaani vikali
shambulizi hilo, ingawa hawajaeleza ni nani wanayemshuku kulifanya.

Chanzo:BBC