MCHUNGAJI Ambilikile Masapila (78) ameibuka na kudai Mungu
amemuonyesha unyayo wa mtu wa 182 tangu kuumbwa kwa Adamu. Masapila
amekuwa maarufu kwa kutoa huduma ya dawa kwenye kikombe iliyodaiwa
kutibu magonjwa sugu. Maelfu ya watu walikwenda kunywa "kikombe hicho
cha Babu" mwaka juzi.
Akiwa ametanguliza sharti la kutopiga picha unyayo huo ulio kwenye
jiwe alilolihifadhi nyumbani kwake, Masapila aliwaambia waandishi wa
habari kuwa Mungu anaendelea kumuonyesha miujiza mingine.
"Nimepata unyayo wa mtu wa kale na Mungu ameniambia mtu huyo ni wa 182
tangu uumbaji wa Adamu na alikuwa binti anayeitwa Tutali.
"Tutali alikanyaga jiwe likazama kama mnavyoona huu ni unyayo wake…
awali Mungu alinionyesha mahali ulipokuwa na akanielekeza nikaenda
kuuchukua.
"Lakini mpaka sasa bado hajazungumza na mimi kwaajili ya kuuweka
hadharani hatua hiyo ni mpaka Mungu atakaponiruhusu," alidai Masapila.
Alipoulizwa kama amewasiliana na wanasayansi waukague na kujiridhisha
kama ni unyayo kweli, alisema hajafanya hivyo kwa vile anaendelea
kumsikiliza Mungu.
"Hamfahamu bustani ya Eden ilikuwa kwenye hili eneo la Ngorongoro.
Niwaombe Watanzania waendelee kusubiri na wenyenia mbaya wataona
maajabu zaidi," alisema Masapila.
Akifafanua kuhusu huduma yake kupungukiwa na watu, Masapila alisema,
mambo mengi yalichangia ikiwamo gharama za kufika nyumbani kwake
kunywa dawa.