Bi Kidude Afariki

Mwimbaji nguli wa muziki wa tarabu nchini Tanzania Fatma binti Baraka,
maarufu kama Bi Kidude amefariki Jumatano kisiwani Zanzibar akiwa na
umri wa zaidi ya miaka 100.
Taarifa ya kifo chake ilitolewa na mjukuu wake Fatuma Baraka ambaye
pia ni muimbaji wa Taraabu. Alisema Bi Kidude alifariki hospitalini
kutokana na maradhi ya kisukari na uvimbe kwenye Kongosho.
Bi Kidude amekuwa katika fani ya muziki wa taarab ya kiasili pamoja na
ngoma za unyago kwa zaidi ya robo tatu ya umri wake.

Katika miaka ya karibuni afya yake imekuwa ikizorota kiasi cha
serikali ya Zanzibar kumzuia kupanda majukwaani kuburudisha japokuwa
alionekana katika tamasha la Sauti za Busara mwezi Februari mwaka huu.
Mipango ya mazishi ya nguli huyu inafanywa nyumbani kwake Zanzibar.

Wengi, hasa vijana wa kizazi kipya wanamfahamu Bi. Kidude kwa uwezo
wake mkubwa wa kuimba taarabu kwa kuchanganya lugha ya kiswahili na
ile ya kiarabu. Nyimbo zake za kiarabu mara nyingi zimekuwa na ladha
kama ile ya aliyekuwa mwimbaji gwiji wa Misri Ummu Kulthumu.
Sio uimbaji tu uliomfikisha Bi. Kidude alipofika, bali uwezo wake pia
wa kutunga mashairi, kutumia ala za mziki kama vile kupiga ngoma na
hata ngoma za unyago, vyote hivi vilimuweka Bi. Kidude katika nafasi
tofauti katika jamii.
Alikuwa na tabia ya kumwita kila mtu 'mwanangu,' ingawa yeye mwenyewe
hakubahatika kupata mtoto. Katika mahojiano aliyofanyiwa na vyombo
mbali mbali vya habari, mwenyewe alisikika akisema, ingawa alikuwa na
hamu ya kupata mtoto, lakini Mwenyezi Mungu hakumjaalia.
Katika miaka ya hivi karibuni, Bi. Kidude alishirikishwa sana na
wasanii wengine katika kazi zao. Miongoni mwao ni Ahmada Amelewa, Fid
Q Juhudi za Wasiojiweza.
Mbali na hayo, mashirika mbali mbali yakiwemo ya kibiashara na yale
yasiyo ya kiserikali yaliona mvuto aliokuwa nao Bi. Kidude katika
jamii, hivyo wakamtumia katika matangazo mbali mbali maarufu likiwa
lile la kutokemeza Malaria.
Ni bibi aliyebahatika kusafiri takriban duniani kote, na vilevile
katikamaisha yake alijinyakulia tuzo lukuki. Miongoni mwa hizo ni ile
ya 2005 WOMEX ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika tasnia ya
muziki.
Katika siku zake za mwisho, Bi. Kidude alikuwa akiumwa, lakini wengi
wanahusisha kuumwa kwake na utu uzima aliokuwa nao.
Kifo chake ni pigo kubwa kwa wote, lakini zaidi ni wanamziki wa kizazi
kipya waliokuwa wakimuona Bi. Kidude ni nyanya yao.