CAG: Aagiza Kumbi za Harusi, M-Pesa,Tigo Pesa na Zinginezo Kutozwa Kodi

MKAGUZI na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh,
ameshauri kampuni za simu zinazotoa huduma ya utumaji fedha na kumbi
za harusi vitozwe kodi. Sambamba na hilo aliutaka uongozi wa Bunge,
kurejesha Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha
taarifa yake bungeni mjini hapa jana akisema uamuzi wa kufuta kamati
hiyo na kazi zake kuunganishwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC),
hautakidhi matarajio ya wadau wa uwajibikaji.
Kwa upande wa kodi, alishauri kodi kutoka kwa wafanyabiashara wadogo,
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ihusishe kikamilifu makatibu kata
kutambua walipa kodi wakiwamo wamiliki wa kumbi za harusi na mikutano.
Akifafanua kuhusu kodi kwenye kampuni za simu za mkononi alitaka
zitozwe kodi ya zuio la malipo ghafi ya kamisheni, inayolipwa kwa
wanaofanya biashara hiyo ya kuhamisha fedha kwa niaba ya kampuni.
Uhamishaji fedha hizo unafaywa kwa kupitia mifumo ya M-pesa, Tigo
Pesa, Airtel Money na Easy Pesa.
Alishauri kodi hiyo ya zuio, ipunguzwe kutoka kodi ya mwisho
inayotakiwa kulipwa na kampuni za simu.
Kamati ya POAC Utouh alisema PAC itazidiwa na wingi na ukubwa wa
majukumu na akatoa mfano, kuwa hata kabla ya kamati hizo kuunganishwa,
kamati hizo mbili zilikuwa zinazidiwa.
Alisisitiza kuwa ni jambo jema POAC irejeshwe kwa jina lolote, lakini
kazi zake zibaki zile zile.
"Kuna mashirika 176, ukiweka na taasisi za Serikali mzigo unakuwa
mkubwa na PAC hii ya Zitto (Kabwe ambaye ni mwenyekiti), kama
atafanikiwa hata nusu ya kazi zake, itakuwa ni muujiza.
"Hivyo nashauri tuone uwezekano wa kurudishakamati hii hata kama
itakuwa na haja ya kubadilisha jina, iitwe ya mashirika ya umma auya
uwekezaji, lakini ifanye kazi za POAC," alisema Utouh. Wabunge na CAG
pia alisisitiza kuwa licha ya Serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya
ukaguzi wa umma, mabadiliko hayo hayajaingilia uhuru wa ofisi yake
kutimiza wajibu wake.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa PAC, alilalamikia sheria hiyo kuwa inawaziba
midomo wabunge kwa vile wanazuiwa kujadili ripoti ya CAG.
Zitto alisema mfumo uliokuwapo wa kuwasilisha ripoti za kamati za
Bunge, umefutwa na Serikali baada ya kutunga sheria, na Serikali
inachotaka ni Bunge kujadili ripoti hizo kupitia kamati zake kabla ya
kujadiliwa na Bunge zima.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema Serikali imetunga
sheria hiyo kwa vile haitaki kusimamiwa na Bunge, ila inataka Bunge
kiwe chombo cha kujadili tu. Alisema hilohalikubaliki na akasisitiza
kuwa kamwe hawataruhusu ripoti za kamati ya CAG isijadiliwe bungeni.
"Tunatumia miezi mitatu kuomba fedha za Watanzania, lakini linakuja
suala la kuhoji matumizi yake kwa sasa tunanyimwa fursa
hii…hatuikubali ni lazima ripoti hizi zijadiliwe namwenye kuwajibika
awajibike kama ilivyotokea mwaka jana," alisema Filikunjombe.
Mwenyekiti wa PAC wa zamani John Cheyo alisema sheria hiyo mpya ya
Ukaguzi wa Umma, inaifedhehesha Serikali na akashauri marekebisho hayo
yafutwe na Bunge ili kutoa fursa ya ripoti ya CAG kujadiliwa.
"Tulikuwa tunakwenda mbele sasa na mabungemengine yalikuwa yanakuja
hapa kujifunza namna tunavyoshirikiana na CAG kusimamia fedha za umma,
lakini sheria hii ya sasa inaturudisha nyuma, tusikubali ni lazima
ripoti hii ijadiliwe bungeni," alisema Cheyo.
Misamaha ya kodi Wakati huo huo, CAG alisema ataanza ukaguzi kwenye
misamaha ya kodi kwa vile fedha ambazo zingelipwa kutokana na
misamaha, ni za Serikali ambazo zinatolewa kama ruzuku kwa wanaopewa
misamaha hiyo.
"Tumeamua kuikagua kwa kina misamaha yote ya kodi kuanzia mwaka ujao
wa fedha kwa madhumuni ya kuangalia manufaa ya misamaha hiyo kwa
uchumi wa Taifa," alisema Utouh.
Lakini CAG alitaka hati za misamaha ya kodi, ziwekwe bayana kuwa
msamaha wa kodi ni wa muda gani, unaanza lini na kumalizika lini.
Alitaka misamaha ya kodi ianishwe ikionesha malengo yanayokusudiwa na
kuwa na utaratibuwa Serikali kusimamia utekelezaji wa misamaha hiyo.
Ameshauri pia mikataba yote yenye vipengele vya misamaha ya kodi,
ipitiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya ushauri kabla ya
kusainiwa na pande husika.
Pia alishauri mikataba ya kuchimba madini, ijadiliwe na Kamati ya
Bunge inayoshughulikia masuala ya madini, na ushauri utolewe kwa
waziri husika kabla ya kusainiwa.



Chanzo:HabariLeo