Viongozi Wa Uamsho Wafutiwa Kesi

MAHAKAMA ya Mwanakwerekwe, Zanzibar imefuta kesi iliyokuwa ikiwakabili
viongozi kumi wa Jumuiya ya Uamsho, visiwani Zanzibar.
Mahakama hiyo, imefikia uwamuzi huo leo, wakati viongozi hao
walipofikishwa Mahakamani hapo.
Kwa hivyo: Kutokana na hatua hio, viongozi hao sasa watakuwa
wanakabiliwa na kesi inayoendelea katika mahakama kuu ya Vuga, mjini
Zanzibar.
Mara ya mwisho viongozi hao wa Dini, walipofikishwa mahakama kuu,
chini ya Jaji Fatma Hamid, kesi yao ilipangwa kusikilizwa tena Aprili
11, mwaka huu.
Jaji Fatma, aliuagiza upande wa mashtaka kupeleka mahakamani kwa
maandishi, ombi la kuzuia kutolewa kwa dhamana kwa washtakiwa hao.
Jaji huyo aliongeza: Licha ya kwamba upande wa mashtaka umekata rufaa
kuzuia kusikilizwa kwa ombi la dhamana, mahakama itaendelea kusikiliza
kesi ya msingi pamoja na dhamana inayohusu viongozi hao.
Upande wa Mashtaka katika kesi hiyo unaongozwa Ramadhan Nassibu na
Raya Msellem, huku upande wautetezi unaongozwa na wakili, Salim Towfiq
na wenzake..