Aua Mkewe baada ya Kumfumania

Mkazi mmoja wa Kijiji cha Idubula, katika Kata ya Karitu ,wilayani Nzega, Tabora, amemuua mkewe kwa kumkatakata kwa mapanga baada ya kumfumania.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Antony Lutta, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa mkesha wa Sikukuu ya Pasaka.
Lutta alisema mtuhumiwa alimfumania mke wake Veronica Maganga (20) akiwa chumbani kwake na mwanamume mwingine .
Kwa mujibu wa kamanda huyo, mwanamume huyo alifanikiwa kukimbia.
Alisema  hasira za mtuhumiwa katika tukio hilo  ziliishia kwa kumtakata mke kwa panga hadi alipokufa.
Kamanda Lutta aliwataka wananchi kutojichukulia sheria mikononi mwao na badala yake, waviachie vyombo vya dola kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa.
“Watu wamekuwa na tabia ya kujichukulia sheria mikononi kwa kuwahukumu watuhumiwa, huo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi na tunawasihi waache,” alisema kamanda huyo.
Alisema mtuhumiwa wa tukio hilo atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa upelelezi.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz