Mvutao Nani Wa Kuchinja Nyama Waendelea

Tunduma ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, baada
kutokea mvutano mkali kuhusu nani anayepaswa kuchinja mifugo bainaya
waumini wa dini mbili; Waislamu na Wakristo.
Mamia ya polisi kutoka wilaya zinazouzunguka Mji wa Tunduma walimwagwa
na walilazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha ili
kuwatawanya waandamanaji pia, kutuliza vurugu zilizodumu kwa zaidi ya
saa nne.
Vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani, zimetokeasiku tatu tu tangu
Rais Jakaya Kikwete aonye kwamba kwamba vurugu zenye sura ya kidini ni
hatari na zinaweza kuvuruga amani na utulivu uliodumu kwa miaka mingi
nchini.
Mijadala kuhusu vurugu hizo ilitawala katika mitandao ya kijamii
ikiwamo facebook, Mabadiliko Forum na Jamii Forums ambako watu
mbalimbali walionyesha kukerwa nazo, huku wakiitaka Serikali ichukue
hatua za kudhibiti.
Kutokana na vurugu hizo zilizoanza saa 4:30 asubuhi,wakazi wa mji huo
walijifungia ndani kwa kuhofia usalama wa maisha yao, huku maduka na
shughuli za biashara nazo zikifungwa.
Mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba
katika vurugu hizo, watu zaidiya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa
Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.
Habari zaidi zinasema barabara za mji huo zilifungwa, umeme ulizimika
baada ya moto kulipuka kwenye moja ya nguzo za umeme. Pia mpaka wa
Tanzania na Zambia ulifungwa kwa muda.
Magari ya abiria na yale ya usafirishaji yaliyokuwa yakitoka na
kuelekea Zambia, Dar es Salaam, Sumbawanga na Mbeya Mjini pia
yalikwama na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria. Msikiti ulivunjwa
na watu wawili akiwamo askari polisi walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumanalithibitisha kutokea
kwa vurugu hizo na kwamba tukio hilo limetokea wakati Serikali ikiwa
kwenye mazungumzo na baadhi ya wahusika katika mgogorowakiwamo
viongozi wa dini na wachinjaji wa nyama.
"Mgogoro wa kuchinja umedumu kwa siku tatu, jana kamati ya ulinzi na
usalama chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ilikutana na
baadhi ya viongozi wa dini na wadau wa kuchinja nyama na kuna mambo
matatu ambayo yalitolewa katika mkutano huo," alisema Diwani.
Alisema katika mkutano huo Kandoro aliagiza kuwa wananchi wanatakiwa
kuwa wavumilivu katika kipindi hiki, ambacho Serikali ngazi ya kitaifa
inalishughulikiana kuwataka kuendelea na hali uchinjaji kama
ilivyokuwa awali na kila mmoja afanye kile anachoamini katika dini
yake wakati wa kula.
Hata hivyo, baadhi ya Wakristo waliafikia lakini wengine hawakuafiki.
Hivyo jana asubuhi walihamasisha maandamano katika mji huo ambayo
yalisababisha vurugu hizo.
"Pamoja na hayo yote uchunguzi wa kitaalamu tumebaini kuwa vurugu hizo
siyo za kidini, bali zimehusishwa siasa kwani hata viongozi wa dini
waliohusika ni baadhi siyo wote ambao wanajishughulisha na suala
hili," alisema Diwani.
source: .mwananchi