Uhuru Kenyatta Aapishwa

Uhuru Kenyatta hii leo ameapishwa kama rais wa nne wa Jamuhuri ya
Kenya kufuatia ushindi wake dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga katika
uchaguzi uliofanyika Machi nne.
Ushindi wake wa kwanza katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo,
ulihalalishwa na mahakama ya juu zaidi nchini Kenya.
Kenyatta na naibu wake William Ruto, wanakabiliwa na kesi katika
mahakama ya uhalifu wa kivita iliyotokana na ghasia za baada ya
uchaguzi mkuu miaka mitano iliyopita.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir, anayekabiliwa na kibali cha kukamatwa na
mahakama ya ICC, hatakuwepo kushiriki sherehe hizo.
Bwana Kenyatta ni mwanawe rais mwanzilishi wa Kenya, Jomo Kenyatta, na
ni mrithi wa mali nyingi sana nchini humo.
Kenyatta aliwahi kuhudumu kama naibu waziri mkuu , waziri fedha,na
waziri wa serikali za mitaa chini ya utawala wa rais
anayeondokamamlakani Mwai Kibaki.
Kenyatta mwenye urmi wa miaka 51, ni rais wa kwanza mwenye umri mdogo
zaidi kuwahi kuongoza nchi hiyo.
Raila Odinga alipinga vikali ushindi wa Kenyatta na hata kuwasilisha
kesi katika mahakama ya juu zaidi.
Baada ya uamuzi wa mahakama uliosema kuwa alichaguliwa kihalali,
Kenyatta alisema kuwa serikali yake itashirikiana na na wakenya
kuhakikisha kuwa wanawahudumia wakenya wote bila mapendeleo.
Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza chini ya katiba mpya na wa kwanza
katika kipindi cha miaka mitano tangu ghasia zilizoshuhudiwa baada ya
uchaguzi wa mwaka 2007.
Bwana Kenyatta anatarajiwa kufika mbele ya mahakama ya ICC kwa kesi
anayokabiliwa nayo, ya uhalifu dhidi ya binadamu.
Amekanusha madai hayo.
Kenya imetia saini mkataba wa Roma unaoishurutisha kutii mahakama ya
ICC mnamo mwaka 2002.
Lakini nchi nyingi za Afrika zimekataa kuitii mahakama hiyo na
hatakutekeleza kibali cha kumkamata rais Bashir anayetakikana na
mahakama ya ICC.