Vigogo Ardhi Wafikishwa Mahakamani

Dar/Korogwe. Maofisa waandamizi serikalini wamefikishwa katika
Mahakama tofauti Dar es Salaam na Korogwe jana wakituhumiwa kwa
makosa ya matumizi mabaya ya ofisi na kuhujumu uchumi.
Maofisa hao wanatoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Wilaya ya
Korogwe.
Kesi ya Dar
Mpimaji wa Wizara ya Ardhi, Revocatus Wachawendera na Mpimaji wa
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Steven Kongwa walifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka
mawili, likiwamo la matumizi mabaya ya ofisi. Kongwa aliwahi kuwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke na alistaafu miaka miwili
iliyopita.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Wakili Hussein Mussa jana alidai mbele ya Hakimu Mkazi,
Augustina Mmbando kuwa washtakiwa hao walifanya makosa hayo kati ya
Januari 2000 na Desemba 2001. Akisomahati ya mashtaka yanayowakabili
washtakiwa hao, Wakili Mussa alidai kuwa washtakiwa hao kwa
pamojawakiwa waajiriwa wa ofisi ya umma, walitumia madaraka yao
vibaya.
Alisema walikiuka mamlaka ya ofisi zao kwa kugawa eneo la wazi
lililopo Mbezi ambalo lilitengwa kwa ajili ya bustani kinyume cha
sheria. Wakili Mussa alidai katika shtaka jingine kuwa maofisa hao kwa
pamoja walikiuka Kifungu cha 35 cha Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa kuligawa eneo hilo.

Alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja katika kipindi hicho cha Januari
2000 na Desemba 2001 wakiwa watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam, kwa makusudi walikiuka sheria hiyo ya mipango miji na kugawa
eneo la Mbezi Kitalu L bila ya kupata kibalikutoka mipango miji. Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana na Wakili Mussa
alisema upelelezi umekamilika, hivyo aliiomba Mahakama kuipangia kesi
hiyo siku nyingine ili kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Ili kupewa dhamana, Hakimu Mmbando aliwataka kila washtakiwa kila
mmoja wao kuwa na mdhamini anayeaminika ambaye anafanya kazi katika
taasisi inayotambulika kisheria.
Sharti jingine ni la kila mdhamini kusaini bondi ya Sh10 milioni.
Washtakiwa walikamilisha masharti hayona kesi yao imeahirishwa hadi
Mei 20, mwaka huu.
Kesi ya Korogwe
Takukuru wilayani Korogwe imewashtaki vigogo watatu kwa makosa manne
likiwamo la kuhujumu uchumi na kusababishia hasara ya Sh56 milioni
kwenye Halmashauri ya Korogwe mkoani Tanga.
Mwendesha mashtaka wa Takukuru, George Magoti alimsomea mashtaka
mshtakiwa wa pili tu, Declley Nyato.
Mshtakiwa wa kwanza, ambaye ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri wa
wilaya hiyo, Christine Midello na mshitakiwa wa tatu, Ofisa Ardhi wa
Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Emmanuel Ntatiye hawakuwapo mahakamani.
Mbali na kumsomea mashtaka, Magoti aliiomba Mahakama ya Wilaya ya
Korogwe kutoa hati zitakazowezesha kukamatwa kwa washtakiwa hao
wengine.
Magoti aliiambia Mahakama kuwa kati ya Julai na Agosti mwaka 2011,
Nyato na wenzake walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kuidhinisha malipo
ya Sh15 milioni kwa Kampuni ya Concise pasipo kuishirikisha Bodi ya
Zabuni.
Katika kosa la pili, Nyato anadaiwa kuruhusu kufanyika kwa malipo ya
Sh41,050,000 kwa Kampuni ya Concise Geo Solution bila ya kuishirikisha
bodi ya zabuni na shtaka la tatu, wote wanatuhumiwa kupanga njama za
kutenda kosa namba moja na mbili.

Shitaka la nne ni la kuhujumu uchumi. Wote kwa pamoja wanadaiwa
kuisababishia Halmashauri ya Mji wa Korogwe, hasara ya Sh56,185,000 na
kuvunja Sheria ya Kuhujumu Uchumi.
Nyato aliyakana mashtaka yote. Hakimu Arnold
Kirekiano aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu baada ya kutoa
masharti likiwamo la kuwa na mdhamini mmoja, ambaye ni mwajiriwa wa
umma au shirika linalotambuliwa ambaye ana makazi ya kudumu Korogwe au
fedha taslimu Sh9.4 milioni au hati ya mali isiyohamishika au maelezo
yatakayothibitisha mali hiyo aliyonayo mdhamini ina thamani sahihi
iliyotajwa na kusalimisha pasi za kusafiria mahakamani.



Chanzo: Mwananchi.co.tz