Teknolojia ya Goli Kuanza Kutumika Ligi Kuu Uingereza

Klabu za ligi kuu soka nchini England zimepitisha sheria ya kutumia
teknolojia ya camera katika maamuzi ya mchezo wa soka kuanzia msimu
ujao.
Kampuni ya Uingereza ya Hawk-Eye imeshinda tenda na kupatiwa mkataba
wa kufunga vifaa maalumu kwenye viwanja vyote 20 vya timu za ligi kuu
nchini England.
Hawk-Eye itafunga kamera saba kwenye kila goli maalumu kwa kutambua
kama mpira umevuka mstari wa goli na kumjulisha mwamuzi wa mchezo huo
kupitia saa yake ya mkononi,na imesemainauhakika hakuna marejeo yoyote
ya matangazo ya picha ambayo yatapingana na maamuzi ya teknolojia
hiyo.
Kampuni hiyo ya Hawk-Eye inajulikana kwa kufunga teknolojia kama hiyo
kwenye mchezo wa Tenesi na Kriketi,ambapo camera maalumu huweza
kutambua iwapo mpira umegusa mstari ama la na kumjulisha mwamuzi na
wasaidizi wake ndani ya sekunde chache.
Chama cha soka nchini England FA,kitafunga vifaa hivyo kwenye uwanja
wa Wembley tayari kwa kutumika kwenye mchezo wa ngao ya jamii hapo
mwezi wa nane mwaka huu.
Vilabu vikubwa vyote nchini England vimepiga kura ya kupitisha maamuzi
hayo katika mkutano wao uliofanyika hii leo jijini London,Huku viwanja
vingine vya timu 17 zitakazosalia ligi kuu na zile 3 zitakazopanda
daraja vitawekewa teknolojia hiyo na shughuli nzima itachukua wiki
sita kukamilika.
Msukumo wa kutumia teknolojia maalumu ya kutambua goli ilipata nguvu
baada England kukataliwa goli lao la kusawazisha walipocheza na
Ukraine,Mchezo ambao England walifungwa bao moja kwa bila kwenye
michuano ya kombe la mataifa barani Ulaya mwaka 2012, Ambapo mwezi
mmoja baadaye bodi ya vyama vya soka vya kimataifa (IFAB) katika kikao
chake mjini Zurich kilipitisha teknolojia mbili ili zitumike kwenye
michezo ya soka.
Nalo shirikisho la kandanda Ulimwenguni FIFA kupitia kwa rais wake
Sepp Blater alisema kukataliwa kwa goli la Frank Lampard kwenye mechi
ya robo fainali kati ya England na Ujerumani mwaka 2010 katika
michuano ya kombe la dunia,kulichangia kwa kiasi kikubwa maamuzi ya
shirikisho hilo kupitisha sheria ya matumizi ya teknolojia ya kutambua
goli.
Chama cha soka cha England kimesema kingependa kuona teknolojia hiyo
inaanza kutumika kwa vitendo haraka iwezekanavyo.