Mji wa Geita na maeneo ya jirani juzi ulikumbwa na taharuki ya aina
yake, pale mwanamke ambaye anadaiwa kwamba alifariki miaka mitano
iliyopita alipoonekana akiwa hai katika eneo la Kasamwa.
Inadaiwa kwamba Flora Onesmo (45) alifariki Februari 28, 2008 katika
Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuzikwa katika Kijiji cha Nakasenya,
Kata ya Butundwe, lakini juzi alfajiri alikutwa ameketi nje ya nyumba
ya dada yake aitwaye Monica James, anayeishi Kasamwa.
Aliyekuwa wa kwanza kumwona Flora ni mdogo wake aitwaye Monica Onesmo
ambaye baada ya kuamka saa 11:00 alfajiri nyumbani kwa dada yake,
alimwona mwanamke aliyekuwa ameketi nje ya nyumba hiyo, lakini
alimfananisha mwanamama huyo na marehemu dada yake.
"Baada ya kumwona nilimwita mtoto wake tunayekaa naye na nikampigia
simu dada (Monica) ambaye alikuwa amelala chumba kingine nikamwambia
kwamba nimeamka na kumkuta mwanamke amekaa hapa nje, lakini kila
nikimwangalia anafanana na marehemu dada yetu,"alisema Jubili na
kuongeza kwamba alipowaita wote walitoka nje.
Alisema mtoto wa Flora (marehemu anayedaiwa kufufuka) anaitwa Rebeka
Elisha (16) na kwamba walimchukua tangu 2008 wakati mama yake huyo
alipofariki dunia katika Hospitali ya Geita ambako alikuwa amelazwa
kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa ini.
Rebeka ambaye ni mtoto wa nne wa Flora alisema: "Mama mdogo alituita
sisi tulikuwa tumelala akasemakwamba nje kuna mwanamke ambaye
anafanana na marehemu mama yetu, ndipo na sisi tukatoka na kweli
kumwangalia alikuwa ni yeye kabisa."
Alisema walipomuhoji mama yake huyo kwamba ametokea wapi, aliwaeleza
kuwa ametoka eneo la Katoro kwa mganga na aliletwa na watu ambao
hakuwatambua Alhamisi saa 1:30 usiku ndani ya gari na watu hao
walimshusha kwa mtu aitwaye Juma Luchunga ambaye ni jirani na dada
zake hao.
Kauli ya Flora
Akizungumza na waandishi wa habari, Flora alisema yeye ni mkazi wa
Katoro na kwamba alitokea Katoro nyumbani kwa mganga wa jadi ambaye
hata hivyo hakumtaja kwa maelezo kwamba wataalamu wake (majini)
wamemkataza.
"Nilikuwa naishi kwa mganga wa kienyeji ila alikuja mwanaume wakati
nikiwa pale akaninywesha dawa kisha tukapakizwa kwenye gari na watu
wawili ambaosikuwatambua, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume mpaka
hapa Kasamwa tukashushwa saa 1:00 jioni,"alisema Flora.
Alisema alipofika Kasamwa alikwenda kunywa uji kwamama mmoja ambaye
pia hakumtaja na kwamba baadaye alipelekwa nyumbani kwa mtu mwingine
saanne usiku, lakini watu wa nyumba hiyo walipomwona walimwambia:
"Hapa si kwako twende tukupeleke kwa ndugu yako" na ndipo wakampeleka
kwa dada yake ambako aliketi nje hadi alfajiri.
Flora alisema kabla ya kuishi kwa mganga alikuwa akiishi porini ambako
alitupwa na watu asiowafahamuna baadaye aliokotwa na wasamaria wema
ambao ndiyo walimpeleka kwa mganga ambako alikuwa akiishi muda wote.