Auza Mtoto Wa Kaka Yake

MKAZI wa kijiji cha Mpemba wilayani Momba, anashikiliwa na Polisi
Mbeya, kwa tuhuma za kuuza mtoto wa kaka yake, ili apate fedha ya
kusaidia kesi ya baba wa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema mwanamke
huyo, Tabu Mwashipete (40), mkulima katika kijiji hicho, alikamatwa
juzi saa 2 usiku akiwa katika harakati za kuuza mtoto huyo, Hosea
Mwashipete (5).
Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, Hosea alikuwa akiuzwa kwa mkazi wa
kijiji cha Mpemba, John Sinyinza (64), kwa gharama ya Sh milioni moja.
Sababu ya kuuza mtoto huyo, kwa mujibu wa Kamanda Athumani, ni
kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia katika kesi inayomkabili baba wa
mtoto huyo, Simon Mwashipete anayekabiliwa na kesi ya mauaji nchini
Malawi.
Kamanda Athuman alisema mama wa mtoto huyo alikwishafariki dunia na
kumwacha Hosea nyumbani kwa shangazi yake huyo, ambaye aliamua kumuuza
ilikupata kiasi hicho cha fedha. Ilidawa tayari mwanamke huyo alipokea
Sh 100,000 na alikuwa katika mazungumzo ya kumaliziwa Sh 900,000
zilizobaki ili amkabidhi Hosea kwa Sinyinza.
Hata hivyo, Kamanda Athumani alisema wakati mwanamke huyo akisubiri
malipo, mteja wa biashara hiyo alitoa taarifa Polisi na kushiriki
mtego uliowezesha kukamatwa kwa mwanamke huyo.
Mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa Polisi wakati taratibu za kisheria
zikiendelea kufanyika, ili afikishwemahakamani.
Wakati huo huo, Kamanda Athuman alisema mchomanyama, mkazi wa Iwambi
Mbeya, Leonard Kanyiki (35), ameuawa kwa kuchomwa kisu kifuani na
mkazi mwenzake Abdul Saiboko (33), katika ugomvi uliozukakwenye kilabu
cha pombe za kienyeji.
Alisema mauaji hayo yalifanyika juzi saa moja usiku katika eneo la
Iwambi, ambapo mtuhumiwa baada yakuona mwenzake amekufa, alijichoma
kisu kichwani kwa lengo la kujiua, lakini hakufanikiwa.
Kamanda Athuman alisema baada ya mtuhumiwa kujichoma kisu, alikamatwa
na watu waliokuwa eneo hilo na kupelekwa katika hospitali ya Rufaa
Mbeya ambako amelazwa na hali yake si nzuri. Chanzo cha ugomvi kati
yao hakijajulikana na uchunguzi unaendelea.