Korea Kaskazini na Syria Kuzungumziwa Kwenye Mkutano wa G8

Migogoro ya Syria na Korea ndiyo itakuwa swala kuu katika agenda ya
mkutano wa nchi za G8 , baadaye hii leo mjini London Uingereza.
Duru zinasema kuwa Japan, inayoshiriki mkutano huo, inatafuta kauli
kali ambayo itaungwa mkono na nchi zote za G8 kuhusu Korea
Korea Kaskazini imekuwa ikitoa vitisho dhidi ya kambi za kijeshi za
Korea Kusini, Japan na Marekani katika eneo hilo.
Mawaziri wa mambo ya nje pia watajadiliana kuhusu mzozo wa Syria baada
ya kukutana na viongozi wa upinzani Jumatano.
Mwandishi wa BBC wa maswala ya kidiplomasia, James Robbins , anasema
kuwa mawaziri wanakubaliana kuwa vitihso vya kivita kutoka Korea
Kaskazini pamoja na maandalizi ya kufanya jaribio la makombora ni
vitisho vibaya sana
''Marekani ina msimamo mmoja na sisi kuhusu Korea Kaskazini ,'' waziri
wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema kwenye mkutano na
waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Korea Kusini imetahadhari pakubwa huku kukiwa na dalili kuwa Korea
Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la kombora lake mpya.
Pyongyang imehamisha makombora mawili pwani mwa nchi. Makombora hayo
yanaweza kwenda umbali wa kilomita 3,000.
Inaarifiwa kuwa huenda kombora hilo likazinduliwa Jumatatu ambayo
itakuwa siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taifa hilo KimIl-sung
Korea Kaskazini imeanza kutoa vitisho vipya baada ya kuwekewa vikwazo
vipya na Umoja wa Mataifa kufutia hatua yake ya jaribio la tatu la
nuklia.