Membe amtaka Rais Banda aache kutapatapa
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
SERIKALI ya Tanzania imetoa msimamo wake kuhusu mgogoro wa mpaka baina
yake na nchi jirani ya Malawi, huku ikitoa onyo kwa Serikali ya nchi
hiyo. Katika msimamo huo, Serikali ya Tanzania imeitaka Malawi
kutoendelea kutumia maji ya Ziwa Nyasa kabla ya mzozo wa kugombea
mpaka kumalizika.
Akitangaza msimamo huo jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alisema Tanzania haipo
tayari kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambako Malawi
imekimbilia.
Membe alisema Tanzania ipo tayari kuendelea na mazungumzo chini ya
jopo la usuluhishi wa migogoro, ambalo mwenyekiti wake ni Rais mstaafu
wa Msumbiji, Joackim Chisano.
Katika jopo hilo yumo Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki na
Rais Mstaafu wa Botswana, Festus Mogae, huku marais wastaafu wa nchi
hizo zenye mgogoro wakiondolewa.
Membe alimshangaa Rais wa Malawi, Joyce Banda kutokana na kitendo
chake cha kutangaza kutokuwa na imani na jopo hilo na badala yake
kufikia uamuzi wa kwenda mahakama ya ICJ na kusema kuwa hatua hiyo
haitamsaidia kupata umiliki wa ziwa hilo.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana, wakati akitoa msimamo wa Serikali
juu ya mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.
"Kabla ya kutoa msimamo wa Serikali, niwakumbushe kwamba mwaka jana
kati ya Novemba 15 na 17, tulikutana hapa Dar es Salaam lakini mkutano
ulimalizika kwa kuelewana na kutoelewana.
"Kutokana na hali hiyo, tulikubaliana wote na kuweka saini kwenda
kwenye jopo la usuluhishi wa migogoro linaloongozwa na marais
wastaafu.
"Katika mkutano huo, iliamuliwa kwamba marais wastaafu wa nchi mbili
zilizo na mzozo wasishiriki, pia tukakubaliana kwamba nchi zote mbili
zisitumie Ziwa Nyasa hadi hapo suluhisho litakapopatikana.
"Wakati tunasubiria kukutanishwa na jopo hilo, upande wa Malawi, Rais
Banda ametangaza kujitoa katika majadiliano hayo kwa sababu kadhaa
ikiwamo kutokuwana imani na jopo pamoja na kudai Tanzania imepokea
nyaraka za siri kutoka kwa jopo hilo, ili kujiandaa kupataushindi wa
madai yao.
"Banda amedai kwamba aliyetupatia nyaraka hizo ni Katibu Mkuu wa
Sekretarieti ya Usuluhishi wa Migogorobarani Afrika, John Tesha ambaye
ni Mtanzania.
"Tunasema hatujapokea nyaraka zozote za siri kutoka kwa Tesha, ili
kuondoa hofu hiyo tayari Tesha ameondolewa nafasi hiyo na nafasi hiyo
kushikwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Leonard Simao wa Msumbiji.
"Pia amedai kuwa Tanzania tumebuni ramani mpya, hili si kweli bali
ramani mpya tulizonazo ni zile zinazotokanana mikoa na wilaya mpya
tulizozianzisha, sasa lazima zionyesha mpaka wao katika Ziwa Nyasa.
"Katika hali kama hiyo tunamchukulia Banda kama mchezaji wa mpira wa
miguu ambaye kabla ya dakika 90 kumalizika, anaamua kuchukua mpira na
kutoka nao nje bila mwamuzi kupuliza filimbi," alisema.
Msimamo wa Tanzania
Membe alisema hatua iliyochukuliwa na Malawi ya kulikataa jopo na
kuamua kwenda katika mahakama ya kimataifa, ni wazi kuwa Rais Banda
amekiuka makubaliano ya pamoja ya mwaka jana.
Hata hivyo Membe ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, alisema Tanzania kamwe
haitakubali kuburuzwa na Malawi katika mzozo huo wakati sheria na
vielelezo vipo.
Membe alisema Tanzania haipo tayari kwenda ICJ hata kama ikiitwa leo
juu ya suala hilo, kabla ya jopo hilo kusikiliza mzozo huo na kutoa
uamuzi wake.
"Tunaiomba Malawi isitafute vurugu badala yake irudi katika jopo la
usuluhishi, kwani kuendelea kufanya hivyoni kutapatapa na kuashiria
madai yake kwamba si ya msingi.
"Namuomba Rais Banda aheshimu jopo la usuluhishi, kwa kuwa marais na
wanasheria wanaosikiliza madai yetu wana uzoefu mkubwa sana, imani
yetu watatenda haki.
"Tunamwomba kwa mara nyingine na ya mwisho kutoendelea kutumia maji ya
Ziwa Nyasa hadi hapo ufumbuzi utakapopatikana," alisema.
Siri za Banda zafichuka
Katika hatua nyingine, Membe alisema ameshangazwa na hatua ya Rais
Banda kuzunguka katika nchi mbalimbali duniani, akiomba msaada ili
kuikabili Tanzania.
Membe alisema katika ziara hizo, Rais Banda amekuwa akikutana na
viongozi wa mataifa makubwa, wakuu wa vikosi na viongozi maarufu
akiilalamikia Tanzania.
"Huyu Rais Banda ametushangaza kweli, yaani wakati tunasubiria jopo
yeye yupo katika mataifa makubwa kutulalamikia, sasa cha ajabu wale
wote aliokutana nao na kuwaeleza wamempigia simu Rais Kikwete wakihoji
kuhusu malalamiko yake.
"Si Rais Kikwete mwenyewe kapigiwa hata mimi nimepigiwa na kuulizwa na
mara zote tumewaeleza tulipofikia na hali ilivyo, pia tumewaeleza
kitendo cha mwenzetu kujitoa na hatua tulizochukua.
"Narudia kusema hii ni dalili za kuanza kutapatapa na mara zote
tunapokuwa tunadai haki yetu katika mipaka tumekuwa tukisingiziwa
kwamba tunapeleka boti, visababu kama hivyo vinafananishwa na madai ya
Rais Banda," alisema.
Hatua zilizochukuliwa Tanzania
Membe alisema kutokana na hali hiyo, tayari Tanzania imepeleka timu ya
wataalamu nchini Ujerumani katika jengo la makumbusho la dunia,
kutafuta nyaraka za Tanzania tangu ilipokuwa ikitawaliwa na wakoloni
ili kuona mipaka halisi.
Alisema tayari wataalamu hao wamekwisha rudi nchini na wamefanikiwa
kupata lundo la nyaraka ambazo zinaihakikishia Tanzania kuibuka na
ushindi katika mzozo huo.
Membe alisema nyaraka hizo zitawekwa hadharani palewatakapofikishana
mahakamani au watakapokutanishwapamoja mbele ya jopo hilo.
Mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi,
umechukua muda mrefu kutatuliwatangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere hadi leo.
Source:Mtanzania