Wanafunzi Waua Mwizi

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Ntuchi wilayani Nkasi mkoani Rukwa
wanadaiwa kumuua kwa kumpiga mkazi wa kijiji cha Ifundwa wilayani
hapa, Ignas Maruku (29) wakimtuhumu kuingia kwenye bweni la wanafunzi
wa kike na kuiba nguo zao mbalimbali, zikiwemo nguo za ndani.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amemweleza mwandishi wa habari
hizi kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 25 mwaka huu saa 6.00mchana
wakati wanafunzi hao wakiwa darasani.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Mwaruanda alisema siku hiyo, mmoja wa
wanafunzi hao wakike ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja
akiwa nje ya madarasa karibu na bweni lao alimwona kijana huyo
akiingia bwenini mwao hivyo alimshtukia na kuanza kupiga kelele.

Inadaiwa ndipo wanafunzi hao wa kike na wa kiume walipotoka darasani
na kuanza kumfukuza mwizi huyo kisha kumkamata na kuanza kumshambulia
kwa mawe, marungu na fimbo hadi akazimia.

Wakati wanafunzi hao wakimsulubu mwizi wao huyo ndipo walimu wao
walipoacha shughuli zao zote shuleni hapo na kukimbilia eneo la tukio
na kuamuru wanafunzi hao watawanyike na kuacha kumpiga mtuhumiwa huyo,
warejee madarasani.

Kwa mujibu wa Mwaruanda, walimu hao walitaarifu polisi ambao kwa
kushirikiana nao walimkimbiza mtuhumiwa huyo katika Hospitali Teule ya
Wilaya hiyo mjini Namanyere, lakini alifariki dunia wakati akipata
matibabu hospitalini hapo.

Kamanda Mwaruanda amedai kuwa mwalimu wa shule hiyo aliyetambuliwa
kuwa Thobias Ndunguru (26) na mkazi wa kijiji hicho cha Ntuchi, Simon
Osayi wanashikiliwa na Polisi kwamahojiano kuhusu mauaji hayo, lakini
hakuna mwanafuzi yeyote anayeshikiliwa hadi sasa huku uchunguzi zaidi
wa tukio hilo ukiendelea.