ZITTO: MAISHA YETU YAPO HATARINI

Siku moja kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha bungeni, ripoti ya uchunguzi wa IPTL kuhusu ufisadi katika akaunti ya Escrow, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe amesema amekuwa akipata vitisho ili kuzuia ripoti hiyo.

Akizungumza jana, Zitto alisema pamoja na vitisho hivyo haogopi kwa kuwa maisha yake ameshayaweka nadhiri siku nyingi.

"Kuna kundi la wahuni kutoka Musoma limeletwa Dodoma likiongozwa na mtu (jina tunalihifadhi) mwenye rekodi ya ujambazi. Hivi sasa anashikiliwa na polisi kwa kukutwa na nyaraka zilizoibwa Ofisi ya Bunge. Usalama wa wajumbe wote wa PAC upo shakani," alisema Zitto.

Aliongeza kuwa kuna vipeperushi vimesambazwa mjini Dodoma kumkashifu lakini havitamsumbua kwa kuwa yeye anataka ukweli ujulikane.

Baadhi ya wabunge jana walionekana na kitabu kilichoandikwa 'mjue Zitto Kabwe kama mtetezi wa wanyonge,' lakini ndani yake kikiwa na mambo ya kumchafua mbunge huyo.

Vitabu hivyo vinaelezwa kusambazwa kwa wabunge katika nyumba zao vikilenga kuonyesha kwamba Zitto hafai kusimamia PAC ambayo hivi sasa inashughulikia escrow.

Wakati Zitto akisema hayo, suala hilo la vitisho jana pia liliibuka bungeni baada ya Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed kueleza kuwa hali ni tete kuhusu usalama wa wabunge kutokana na escrow.

Akiuliza swali la nyongeza, Mohamed alisema usalama wa wabunge uko shakani kuanzia maeneo wanayofanyia kazi na makazi yao na hasa kipindi hiki tangu kuanza kwa sakata la escrow.

"Je, nini tamko la Serikali juu ya ulinzi na usalama wa wabunge katika maeneo ya kazi, pia katika maeneo yao ambayo wanaishi?" alihoji.

Kabla ya majibu kutolewa na Serikali, Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye jana alianza kuongoza vikao baada ya safari yake nje ya nchi, aliingilia kati akisema ofisi yake inakusudia kujenga kijiji cha wabunge ambako watalindwa kwa pamoja.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba alisema Serikali inafanya tathmini ya vitisho vyote vya viongozi nchini wakiwamo wabunge ili kuhakikisha wanakuwa salama.

Chanzo: Mwananchi