Aidha, mahakama hiyo imewaachia huru washitakiwa wengine wawili wa kesi hiyo, polisi wa upelelezi, Shaaban, F 7769, na polisi wa kike mpelelezi, Neema, F 6545, baada ya kuwakuta hawana hatia.
Hukumu hiyo ya kesi namba 16 ya mwaka 2013, ilitolewa jana mjini hapa na Jaji Rose Temba, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewana pande zote mbili.
Awali, ilielezwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali, Archiles Mulisa akisaidiwa na Catherine Paul kuwa washitakiwa walifanya mauaji ya kukusudia Februari 14 mwaka 2012 kinyume cha Kifungu Namba 196 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa Marejeo mwaka 2002.
Mulisa alidai washitakiwa hao kwa pamoja walihusika na mauaji ya Daniel Mwakyusa baada ya kumpiga kwa kutumia silaha inayodhaniwa kuwa ni bunduki, njeya ukumbi wa starehe wa Universal uliopo Uyole jijini Mbeya.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Jaji Temba alisema anawaachia huru mshitakiwa namba mbili, Shaaban ambaye alikuwa dereva wa gari ya polisi kwa kuwa ushahidi uliotolewa, unadhihirisha kuwa alibaki ndani ya gari akimsubiri mshitakiwa namba moja aliyeshuka na kuingia kwenye ukumbi wa Universal.
Kwa upande wa mshitakiwa namba tatu, Neema, Jaji Temba alisema aliridhishwa na mshitakiwa huyo kutohusika na mauaji kwa kuwa siku ya tukio alikuwa akijisikia vibaya, hivyo alilazimika kubaki na dereva kwenye gari.
Jaji Temba alisema mshitakiwa namba moja, Maduhu, anahusika moja kwa moja na mauaji hayo, kutokana na ushahidi wa kimazingira, kwani yeye ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuondoka na Daniel Mwakyusa eneo la tukio na kumpeleka kwenye gari.
Alisema sababu ya pili, ushahidi ulionesha kuwa silaha yake pekee ndiyo iliyotumika, tofauti na za askari wengine kwa kuwa risasi tatu zilionekana kupungua kati ya zile alizokabidhiwa sambamba na ushahidi wa maganda matatu ya risasi, yaliyookotwa eneo la tukio.
Jaji Temba alisema sababu ya tatu ni kuwa ushahidi uliotolewa, unaonesha kuwa mshitakiwa huyo alikuwa wa mwisho kurejesha silaha, hivyo kuhusishwa moja kwa moja na mauaji hayo.
Alisema kutokana na sababu hizo, mahakama inamtia hatiani kwa kuua kwa kukusudia, hivyo mshitakiwa Maduhu, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Awali, ilidaiwa kuwa siku ya tukio ilikuwa Siku ya Wapendanao (Valentine's Day), ambapo mtuhumiwa akiwa doria na askari wenzie, alimkuta Daniel Mwakyusa akiwa kwenye eneo la starehe na mwanamke anayesadikiwa kuwa alikuwa pia na mahusiano na askari huyo.
Chanzo: Habari leo