UFAULU DARASA LA SABA JUU, MPANDA YAONGOZA WILAYA 10 BORA

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2014 yanayoonesha kuwa, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 6.38 huku Kanda ya Ziwa iking'ara kwa kuwa na shule nane kati ya kumi bora kitaifa.

Shule nyingine mbili zinazokamilisha kumi bora ni za mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro. Aidha, mwanafunzi bora kitaifa ametajwa kuwa ni Rolly Gedi Mabura wa Shule ya Twibhoki ya Mara aliyepata alama 243 kati ya alama 250.

Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde alisema wanafunzi451,392 kati ya 792,118 waliofanya mtihani wamepata jumla ya alama 100 na zaidi kati yaalama 250, ambayo ni sawa na asilimia 56.99 ambapo mwaka janaufaulu ulikuwa asilimia 50.61.

Hata hivyo, alisema wanafunzi 340,726 wamefeli mtihani huo kwa kupata madaraja ya D na E. Alisema wasichana wamefanya vizuri kuliko wavulana ambapo wanafunzi 224,909 sawa na asilimia 60.87 ni wasichana na 226,483 ambayo ni asilimia 53.59 ni wavulana.

Msonde alisema miongoni mwa wanafunzi waliofaulu wenye ulemavu ni 795 (wasichana 355 ambayo ni asilimia 44.65 na wavulana 440 sawa na asilimia 55.35.)

Akizungumzia ufaulu katika madaraja mbalimbali ni kuwa wanafunzi 10,331 (asilimia 1.30) wamepata Daraja A, Daraja B ni wanafunzi 98,789 (asilimia 12.47) na Daraja C ni wanafunzi 342,272 (asilimia 43.21) wakati waliopata Daraja D ni 321,939 asilimia 40.64na Daraja E ni wanafunzi 18,787.

Watahiniwa 792,122 kati ya 808,085 wa Shule za Msingi walisajiliwa kufanya mtihani, walifanya mtihani huo uliofanyika Septemba 10 hadi 11, 2014.

Aidha, alisema takwimu za matokeo zinaonesha ufaulu katika masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 0.64 hadi 8.94 ikilinganishwa na mwaka jana, huku watahiniwa wakifaulu zaidi somo la Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 69.70 na kiwango cha chini zaidi ni Hisabati ambayo ufaulu wake ni asilimia 37.56.

Kiingereza ni asilimia 38.84, Maarifa ya Jamii asilimia 57.33 na Sayansi asilimia 54.89.

Shule Bora Msonde alitaja shule kumi bora kitaifa kuwa ni Twibhoki (Mara), Mugini, Peaceland na Alliance (Mwanza), Kwema (Shinyanga), St. Severine (Kagera), Rocken Hill (Shinyanga), Tusiime (Dar es Salaam), Imani (Kilimanjaro) na Palikas (Shinyanga).

Alisema mikoa kumi iliyofanya vizuri kitaifa ni Dar es Salaam ambayo imeongoza, Kilimanjaro, Mwanza, Iringa, Arusha, Tanga, Njombe, Kagera, Geita na Mtwara wakati wilaya zilizofanya vizuri kitaifa zimeongozwa na Mpanda Mjini (Katavi) na kufuatiwa na Biharamulo (Kagera), Halmashauri ya Moshi (Kilimanjaro), Kibaha (Pwani), Halmashauri ya Arusha (Arusha), Kinondoni (Dar es Salaam), Korogwe Vijijini (Tanga), Ilala (Dar es Salaam), Iringa (Manispaa) na Mji wa Makambako (Njombe).

Aidha, alisema Baraza limefuta matokeo ya mtahiniwa mmoja aliyebainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo ukilinganisha nawatahiniwa 13 wa matokeo ya mwaka jana.

"Baraza linachukua fursa hii kuzipongeza Kamati za Uendeshaji Mitihani za mikoa, wilaya na walimu waliosimamia mtihani hii kwa kuzingatia ipasavyo kanuni za usimamizi wa mitihani ya taifa,"

Waliopata alama za juuMsonde alisema watahiniwa 7,600 wamepata alama 50/50 katika somo la Kiingereza, wanafunzi 32 somo la Kiswahili na hisabati ni wanafunzi 34 ambapo wasichana ni wanane na wavulana 26.