Helikopta hiyo aina ya Robertson R44 yenye thamani ya Dola za Marekani 500,000 (Sh milioni 800), ilitolewa msaada na Taasisi ya Howard Buffet kwa ajili ya kusaidia mapambano hayo.
Ajali ya helikopta hiyo iliyokuwa ikimilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), ilitokea jana saa 4:00 asubuhi maeneo ya Kipunguni B, Moshi Bar, wilayani Ilala, wakati ilipokuwa katika ukaguzi wa kawaida.
Akizungumza katika eneo la ajali, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana na upelelezi unaendelea kujua chanzo.
Kamanda Kova aliwataka wananchi na wakazi wa eneo hilo, kutosogea karibu na mabaki ya helikopta hiyo, ili kuepusha madhara makubwa zaidi yanayoweza kutokea kutokana na kuwepo kwa viashiria vya moto.
"Tunaomba msisogee karibu na eneo hili la ajali, panaweza kulipuka hapa na kusababisha madhara makubwa zaidi, tuchukue tahadhari na tukae mbali na eneo hili," alisema Kova.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidi (ACP), Hamis Suleiman, alitaja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Mrakibu waPolisi Kapteni Kidai Senzala, Mkaguzi wa Polisi Kapteni Simba Musa, Konstebo wa Polisi, Josso Selestine na Kapteni Joseph Khalfan.
Helikopta hiyo ilikuwa na namba 5H- TWA. Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alipongeza wananchi hao kwa kutoa taarifa mapema zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza madhara.
Hata hivyo Sadiki alitaka wananchi kutokimbilia maeneo ya tukio la ajali kama hizo zinapojitokeza kwani kuna uwezekano mkubwa wa wao kupata madhara yanayoweza kusababishwa kulipuka kwa chombo hicho.
Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema waliona helikopta hiyo ikiyumba na kutoa mngurumo usio wa kawaida na baadaye ikazima ambapo rubani alijaribu kuiwashwa bila mafanikio, lakini baadaye ilianguka.
"Tulisikia mlio wa helikopta usio wa kawaida na baadaye ilizima na kusikika tena ikiwashwa ikagoma ndio baada ya muda mfupi, tukasikia kishindo kikubwa cha helikopta hiyo kuanguka," alisema shuhuda huyo.