Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Wakati Waziri Muhongo akitajwa kuwa na uhusiano wa karibu na mtuhumiwa huyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye jana ilikuwa ni siku yake ya kwanza kuongoza Bunge tangu lianze Novemba 4, mwaka huu, anadaiwa kutajwa kuwamo katika orodha ya vigogo waliovuna fedha hizo, huku yeye akipata mgawo wa Dola zaMarekani milioni moja.
Aliyemtaja Waziri Muhongo kuwa na uhusiano wa karibu nakijana huyo, ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Mnyika alimtaja Waziri Muhongo, wakati akichangia mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, bungeni jana.
Muswada huo uliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni, Ijumaa wiki iliyopita."Mheshimiwa Spika, ni muhimu ofisi yako ifuatilie. Kwa sababu mtuhumiwa yule ana uhusiano wa karibu sana naProf. Sospeter Muhongo, ambaye ni mmoja wa watuhumiwa kwenye kashfa tunazozijadili," alisema Mnyika.
Aliongeza: "Sasa nasema haya mapema ili isifikie hatua tukatumiwa kisingizio cha mambo kuwa mahakamani kushindwa kuwataja kwa majina wahusika. Polisi wafanye uchunguzi, wachukue hatua."
Mnyika alisema uharamia kwenye suala IPTL wa muda mrefu umezidi mipaka.
Alisema taarifa alizonazo ni kwamba, polisi wanamshauri Spika wa Bunge kwa sababu wanataka haraka haraka wamkimbize mtuhumiwa huyo mahakamani ili baada ya hapo alieleze Bunge kuwa kishapelekwa mahakamani, hivyo hakuna sababu ya kutaja jina wala suala lake kujadiliwa.
Mnyika alisema tangu siku waliyowapa polisi taarifa, mpaka leo wamekuwa wakisitasita wakishindwa kutaja jina la mtuhumiwa, huku wakisingizia uchunguzi.
Hata hivyo, alisema upande waserikali wanapokutana nao kwenye korido wamekuwa wakiwaambia kuwa mhusika anafahamika, ikiwa ni pamoja na watu wote ambao amekuwa akiwasiliana nao.
"Mheshimiwa Spika, ukiendelea kuyakinga mambo haya kwa kisingizio cha mambokuwa polisi, halafu baadaye polisi wakaenda mahakamani, ukaja kuyakinga hapa kwa kisingizio cha kwamba mambo yako mahakamani, maana yake Mheshimiwa Spika na wewe utahesabika kwamba, hizo mbinu za hao maharamia waliopora ripoti ndani ya ofisi yako pengine na ofisi yako inahusika," alisema Mnyika.
Alimshauri Spika Makinda kuwasiliana na vyombo vinavyohusika ili ofisi yake na kiti chake visitumiwe na watuhumiwa kuficha uharamia unaoendelea dhidi ya Bunge na uwajibikaji, ambao Bunge linapaswa kuusimamia kwa niaba ya wananchi.
Madai hayo ya Mnyika yalitolewa siku moja baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, kukaririwa akisema kuwa katika mahojiano na polisi, kijana huyo alikiri kwamba, alipewa ripoti hiyo na Mbunge mmoja, ambaye alikataa kutaja jina lake ili kuepusha kuharibu upelelezi.
Vijana hao walikamatwa na polisi Jumamosi wiki iliyopita, mjini hapa, baada ya kukutwa wakiwa na ripoti hiyo yenye mhuri wa Katibu wa Bunge, ambayo wanadaiwa 'kuichakachua' kabla ya kuidurufu na kuisambaza mitaani kama njugu.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, pia alithibitisha kutoa taarifa polisi kuhusu vijana hao kumiliki nyaraka zenye muhuri wa ofisi yake isivyo halali.
Kamanda Misime alisema hadi juzi vijana hao walikuwa wanashikiliwa na polisi.
Chanzo: Nipashe