YAMETIMIA ESCROW

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imependekeza kutenguliwa kwa nyadhifa na kuwajibika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baadhi ya mawaziri kutokana na sakata la fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.

Mbali ya mapendekezo hayo, Kamati hiyo imependekeza pia wote waliochukua fedha kutokana na kashfa hiyo iliyohusisha Sh bilioni 306, wafilisiwe mali zao na kushitakiwa mahakamani.

Wanaotajwa kutakiwa kutenguliwa kwa nyadhifa zao mbali ya kuwajibika kwa Pinda ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Naibu wake, Stephen Maselle, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliachim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Kamati hiyo ilitoa mapendekezo yake hayo kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Akisoma maoni na mapendekezo yaKamati baada ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe kusoma sehemu ya uchambuzi wa sakata hilo, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema kwa uzito na unyeti wa suala hilo, Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuwajibika kwa kauli zake na kwa kutotekeleza wajibu wake wa kikatiba ipasavyo, ilikurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao na viongozi wao wa kisiasa.

Kwa mujibu wa Filikunjombe, baadaya kupitia vielelezo vilivyomo katikaripoti ya CAG, "Kamati imejiridhishapasipo mashaka kuwa, Waziri Mkuu alikuwa na taarifa zote kuhusu mchakato mzima wa kuchotwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow."

"Ushahidi ulioletwa na Ofisi ya CAG kwenye Kamati unaonesha kuwa Waziri Mkuu alikuwa akipata taarifa za jambo hili. "Na Kamati imesikitishwa kuona kuwa Waziri Mkuu hakuchukua hatua zozote kuzuia muamala huu usifanyike," aliongeza Makamu Mwenyekiti huyo, na kubainisha kuwa Pinda pia aliwahi kunukuliwa akisema fedha za Escrow si za umma.

Kuhusu Profesa Muhongo, Kamati ilieleza kuwa alifanya udalali wa kuwakutanisha Harbinder Sethi na James Rugemalira (waliokuwa wamiliki wa Independent Power Tanzania Limited) na kuwa alilipotosha Bunge kuhusu fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwamba ndani ya fedha hizo, hakukuwa na fedha za umma."

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, aidha kwa makusudi, ama kwa sababu anazozijua vizuri zaidi mwenyewe, Waziri wa Nishati na Madini ananukuliwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge, kwa nguvu kubwa na kwa kujiamini, akitetea uchotwaji wa fedha hizo kinyume cha masharti ya mkataba wa Escrow," alisema Filikunjombe.

Alisema iwapo waziri huyo angetimiza wajibu wake kidogo tu na ipasavyo, fedha za Tegeta Escrow zisingelipwa kwa watu wasiohusika na nchi ingeweza kuokoa mabilioni yaliyopotea kama Kodi ya Ongezekola Thamani (VAT), Capital Gain Tax na ushuru wa stempu ambazo ni sawa na takribani Sh bilioni 30.

"Kamati inapendekeza kuwa mamlaka yake ya uteuzi, itengue uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na sababu zilizoelezwa," alisema.

Akimzungumzia Maselle, Filikunjombe alisema Kamati imethibitisha kuwa alisema uongo bungeni kwa kutamka kauli ambazo zilikuwa na lengo la kupotosha umma kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow, ikiwemo kutoa kauli ambazo zingeweza kusababisha nchikuingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia na nchi ya Uingereza.

"Kamati inapendekeza kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini)achukuliwe hatua kali za kinidhamu,ikiwemo kutenguliwa uteuzi wake.
"Kamati pia inapendekeza kuwa Naibu Waziri huyu afikishwe mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili ili aadhibiwe kama mbunge kwa kusema uongo bungeni ili liwe fundisho kwa wabunge wengine kuhusu kauli wanazotoa ndani ya Bunge lako tukufu," aliongeza Filikunjombe

Kuhusu Mwanasheria Mkuu Jaji Werema, Kamati ilisema imethibitisha kuwa alitoa ushauri ulioipotosha Benki Kuu ya Tanzania kuhusu hukumu ya Jaji John Utamwa kwa kutumia madaraka yake vibaya.

Alisema Jaji Werema aliagiza kodi ya Serikali yenye thamani ya Sh bilioni 21 isilipwe na hivyo kuikosesha Serikali mapato adhimu."

Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwakujua na kwa makusudi alilipotosha Bunge na Taifa kwamba mgogoro uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow ulikuwa ni mgogoro wa wanahisa wa IPTL badala ya mgogoro kati ya Tanesco na IPTL.

"Kamati inapendekeza kuwa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali utenguliwe na mara moja afikishwe mahakamani kwa matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababisha Serikali kupoteza mabilioni ya fedha," alisema Filikunjombe.

Akimzungumzia Katibu Mkuu Maswi, Makamu Mwenyekiti huyo wa PAC alisema Kamati inapendekeza uteuzi wake utenguliwe na Takukuru wamfikishe mahakamani mara moja, kwa kuikosesha Serikali mapato na matumizi mabaya ya ofisi na kusaidia utakatishaji wa fedha haramu.

Kamati ilisema imethibitisha Maswi amefanya uzembe wa hali ya juu wakushindwa kujiridhisha kuhusu masharti ya sheria ya kodi, na pia imebaini kuwa hakujiridhisha uhalali wa Kampuni ya Mechmar kuuzwa kwa Piperlink na baadaye kuuzwa kwa PAP, na hivyo kusababisha fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kulipwa kwa asiyestahili kinyume cha mkataba wa akaunti ya Escrow.