NUSU YA WABUNGE WACHOKWA MAJIMBONI

KARIBU nusu ya wabunge wa majimbo yote ya uchaguzi nchini, wapo hatarini kuangushwa na wapigakura wao katika katika uchaguzi mkuu wa mwakani, kutokana na kutotekeleza ahadi walizotoa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Asilimia 47 ya Watanzania wote, wameweka wazi kutowapigia kura wabunge wao, kutokana na kushindwa kuzitekeleza au kuzitekeleza kwa kiwango kidogo ahadi, walizotoa wa kampeni za uchaguzi.Ahadi hizo zilihusisha kuboresha barabara, miradi ya maji, kujenga hospitali na zahanati, kuboresha elimu, umeme, mikopo kwa vikundi, kuongeza ajira kwa vijana, kujenga madaraja, kuboresha kilimo na kadhalika.

Hayo yamebainishwa katika ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza, iliyotolewa jana katika mdahalo ulioandaliwa na taasisi hiyo, ambao uliwakutanisha wachambuzi mbalimbali, uliokuwa na mada ya 'Tanzania Kuelekea 2015'.

Kwa mujibu wa utafiti huo, ambao hufanyika kwa njia ya simu, wapiga kura wanane kati ya 10 ambayo ni sawa na asilimia 79, bado wanakumbuka ahadi walizotoa wabunge wao wakati wa kampeni, ambapo wabunge wengi walitoa ahadi za miradi ya ujenzi, miradi ya maji, hospitali, uboreshaji wa elimuna kuongeza madarasa kama vipaumbele vyao.

Akifafanua ripoti hiyo, Mtafiti wa taasisi hiyo, Elvis Mushi alisema kitukibaya ni kuwa ni mwananchi mmoja kati ya wanane ambao ni sawa na asilimia 12, ndiye aliripoti kuwa mbunge wake ametekeleza ahadi zote.

Hata hivyo, Mushi alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kina nafasi ya kushinda uchaguzi japo kwa asilimia ndogo. Alisema takwimu zinaonesha kama uchaguzi ungefanyika Septemba mwaka huu CCM ingeibuka kidedea.

"Sauti za Wananchi iliuliza kama uchaguzi ungefanyika leo, mgombea wa chama gani ungempigia kura, kwa mwaka 2014 asilimia 51 walisema CCM, asilimia 23 Chadema na asilimia 16 walisema wanampigia mgombea na siyo chama," alisema Mushi.

Aidha takwimu za utafiti huo, zinaonesha hata kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ukisimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya Urais, bado haitaweza kuiangusha CCM, kutokana na nusu ya wahojiwa ambao ni asilimi 47 walijibu kuwa wangeipigia kura CCM huku asilimia28 walijibu wangeipa kura Ukawa.

Baada ya kutolewa ripoti ya utafiti huo, ambayo pia iligusa maeneo ya utendaji wa viongozi, changamoto zinazolikabili taifa, ushindani wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM, Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema kumekuwa natabia ambayo imefanywa kuwa ni yakawaida na kubeza maoni ya tafiti kama hizo, jambo ambalo si sawa.Alisema kuwa maoni hayo, yana ukweli ndani yake na pia yanaakisi mawazo ya jamii juu ya mambo mbalimbali, ikiwemo utendaji wa viongozi wao na pia changamoto wanazotaka zitatuliwe.

"Takwimu hizi ziwe ni jicho la kuangalia matatizo yetu na kuondokana na mambo ambayo yamekuwa ni kero kwetu. Ni masuala ya msingi yanayowakera wananchi kwa sababu ni matatizo yale yale ambayo tulianza nayo tangu kipindi cha uhuru, maradhi, umasikini na ujinga," alisema.

Aidha, alitaka vyama vya siasa vikaena kutafakari kwa kuangalia hizo takwimu, kwani zimeonesha kuna mmomonyoko wa kukosa imani na vyama hivyo, jambo ambalo alisema si zuri.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, kuongezeka kwa imani ya wananchi kwenye taasisi za siasa kuliko kwa mtu binafsi ni jambo zuri kwa kuwa inaonesha ustawi mzuri wa demokrasia.

Wakati Nape akiwakilisha chama chake akiyasema hayo, vyama vya Chadema na CUF vilivyoalikwa, havikuwa na wawakilishi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Twaweza, Rakesh Rajani, walituma pia mwaliko kwa vyama hivyo, ingawa walishindwa kuhudhuria mdahalo huo, kutokana na sababu mbalimbali walizozitoa.

Alisema waliwasiliana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa ajili ya kumpa mwaliko huo, ambapo hata hivyo, katibu huyo inaelezwa alijibu kwa sasa viongozi wa chama hicho wamebanwa na shughuli za mikutano inayofanyika mikoani, huku kwa upande wa CUF ukikubali na kutuma mwakilishi, ambaye pia baadaye alitoa udhuru.

"Chadema walisema hawawezi hata kutuma mwakilishi, lakini CUF, Profesa Lipumba alisema atawakilishwa na Naibu Katibu MkuuBara, Magdalena Sakaya ambaye hata hivyo jana (juzi) alituma taarifakuwa asingefika angetuma mwakilishi. "Lakini mwakilishi wa CUF ambaye tuliambiwa angekuja leo (jana) asubuhi, alitoa taarifa amepata dharura hivyo hataweza kufika katika mdahalo huu, hiyo ndiyo sababu mnaona wawakilishi wa vyama vingine hawapo hapa," alisema.

Gazeti hili liliwatafuta viongozi wanaounda Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR na NLD ili kuzungumzia utafiti huo, lakini mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni hawakuweza kupatikana kupitia simu zao za mkononi.


Chanzo: Habari Leo